• HABARI MPYA

    Friday, July 28, 2017

    YANGA B YAIPIGA 3-0 MBEYA CITY NA KUTANGULIA FAINALI

    Na Muhiddin Sufiani, MBEYA
    TIMU ya Vijana ya Yanga U20 jana iliwashangaza mashabiki wa soko waliojitokeza kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuacha gumzo baada ya kuwaduwaza Mbeya City wanaoshiriki Ligi Kuu Bara kwa kuwachapa mabao 3-0 katika mchezo wa Hisani wa kuchangia Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI.
    Mechi hizo za Hisani zimeandaliwa na Tume ya Taifa ya kudhibiti Ukimwi Tanzania TACAIDS, ambapo zinashirikisha jumla ya timu Nne za Yanga U20 na Simba U20 kutoka jijini Dar es Salaam, huku Mbeya City na Tanzania Prisons zikiwa ni zile zinazoshiriki Ligi Kuu Bara.
    Kabla ya mchezo huo kuanza wakati timu zikipasha misuli, mashabiki waliokuwapo uwanjani hapo baadhi walisikika wakijutia kuingia uwanjani kwa kuhisi kukosa burudani, lakini kadri mchezo ulivyokuwa ukiendelea baadhi ya mashabiki walianza kubadilika na kuanza kuwashangilia vijana hao wa Yanga U20, waliokuwa wakionyesha kandanda safi na kuwainua vitini mashabiki wa Soka wa jiji la Mbeya.
    Kiungo wa Yanga B, Said Mussa (kulia) akijaribu kumtoka beki wa Mbeya City, Erick Kyaruzi, 
    Mshambuliaji wa Yanga B, Paul Godfrey, (kulia), akimtoka mchezaji wa Mbeya City, Anthony 

    Katika mchezo huo uliokuwa wa kuvutia tayari Yanga wametangulia fainali na kusubiri mshindi wa mchezo wa leo kati ya Simba U20 na Tanzania Prisons ambapo fainali hiyo itachezwa siku ya Jumamosikwenye Uwanja wa Sokoine.
    Mabao ya Yanga yalifungwa na Maka Edward, katika dakika ya 30 kipindi cha kwanza, akimalizia pasi nzuri ya Said Mussa na dakika ya 64 kipindi cha pili kwa mkwaju wa penati, baada ya kipa wa Mbeya City, Fikirini Bakari, kumchezea rafu mshambuliaji wa Yanga,Paul Godfrey, ndani ya eneo la hatari, huku pazia la mabao likifungwa na Festo Greyson, katika dakika ya 79 baada ya kazi nzuri ya Paul Godfrey, aliyemtoka beki wa kushoto wa Mbeya city na kupiga krosi nzuri iliyozaa bao hilo.
    Akizungumzia matokeo hayo Kocha msaidizi wa Mbeya City Mohamed Kijuso, alisema kuwa kwa upande wake amechukulia ni matokeo ya kawaida na kutokana na kwamba hakuna wanachopoteza bali ilikuwa ni kipimo tosha kwa wachezaji wake ambao baadhi ni wageni waliojiunga na timu msimu huu kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu na kuongeza kuwa ameona mapungufu mengi ambayo atayafanyia kazi na Kocha mkuu atakayejiunga na kikosi hicho.
    ''Kikubwa ni mazoezi kwani tayari nimeona mapungufu ndani ya kikosi changu, nitayafanyia kazi na Kocha atakayejiunga nasi hapo baadaye, ila mashabiki watambue kuwa haya ni matokeo tu ya mchezo na hakuna atulichopoteza kwani ulikuwa ni mchezo wetu wa kwanza kujiandaa na kuangalia kikosi chetu kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu''. alisema Kijuso.
    Kwa upande wake Kocha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa amefurahishwa na matokeo hayo ambayo alikuwa akiyatarajia baada ya kuona wapinzani wake wamepanga Kikosi cha Ligi Kuu, huku yeye akiwaamini na kuwapa majukumu Vijana wa U20, ambao hawakumuangusha baada ya kufuata maelekezo waliopewa.
    ''Kwa kweli Vijana wangu wamenifurahisha sana na matokeo haya kwa upande wangu kama mwalimu niliyatarajia na hasa baada ya kuona wapinzani wakiwa na kikosi cha wachezaji wanaoshiriki Ligi Kuu, kwani nilijua watacheza kwa kuwazania vijana wangu na kujiamini sana jambo ambalo vijana wangu walilitumia kuwashangaza na hawakuamini kilichowakuta katika dakika 90 za mchezo,
    Mimi nilikuwa na vijana wawili tu walicheza ligi msimu uliopita na mmoja ambaye amepandishwa msimu huu, lakini niliwaamini zaidi vijana na kuwapangia Mhilu tu aliyeshiriki ligi iliyopita ili kuwapa hamasa wenzake jambo ambalo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa'', alisema  Nsajigwa
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA B YAIPIGA 3-0 MBEYA CITY NA KUTANGULIA FAINALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top