• HABARI MPYA

    Monday, July 31, 2017

    KESI ZA AKINA MALINZI, AVEVA, KABURU ZAAHIRISHWA TENA LEO KISUTU

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KESI inayowakabili viongozi wakuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Rais Jamal Malinzi na Katibu weke, Selestine Mwesigwa imeahirishwa tena hadi Agosti 11, ili kupisha upepelezi zaidi.
    Mapema hii leo, wawili hao pamoja na Mkurugenzi wa Fedha wa TFF, Isinde Isawafo Mwanga walifikishwa tena mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni mara ya nne na kusomewa mashitaka yao 28, kabla ya kesi hiyo kupelekwa tena mbele hadi Julai 31.
    Hakimu mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Wilbroad Mashauri, alisema anaiahirisha kesi hiyo tena kwa sababu upelelezi haujakamilika na washtakiwa wanarudi rumande hadi Agosti 11 kesi hiyo itakapotajwa tena.
    Malinzi, pamoja na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
    Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
    Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguurma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
    Lakini kwa mwenendo wa kesi, Malinzi ndiyo kama amekwishaaga TFF, kwani uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma naye hajashiriki usaili wa wagombea, hivyo haruhusiwi tena kugombea.  
    Wakati huo huo: Kesi zinazowakabili viongozi wa klabu ya Simba, Rais Evans Eilieza Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ nayo imeahirishwa hadi  Agosti 7, mwaka huu kwa sababu pia upelelezi haujakamilika. 
    Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wapo rumande gereza la Keko tangu Juni 29.
    Wawili hao leo waliletwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam kwa mara ya nne na kusomewa tena mashitaka hayo kabla ya Hakimu Victoria Nongwa kuiahirisha tena kesi hiyo hadi Agosti 7, mwaka huu.
    Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
    Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
    Shtaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya  Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha  likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KESI ZA AKINA MALINZI, AVEVA, KABURU ZAAHIRISHWA TENA LEO KISUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top