• HABARI MPYA

  Saturday, July 15, 2017

  MBARAKA YUSSUF, SHAABAN IDDI NJE WIKI TATU AZAM

  Na Sheekha Jamal, DAR ES SALAAM
  WASHAMBULIAJI chipukizi wa Azam FC, Shaaban Idd Chilunda na Mbaraka Yussuf Abeid wanatarajiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki tatu kila mmoja kufuatia matibabu waliyofanyiwa nchini Afrika Kusini kwa matatizo tofauti.
  Daktari Mkuu wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba, wachezaji hao waliopata mataatizo hayo wakiwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwenye michuano ya Kombe la COSAFA wiki mbili zilizopita nchini humo, walilazimika kubaki Afrika Kusini kwa uchunguzi zaidi.
  Mwankemwa amesema wawili hao walifanyiwa uchunguzi katika Hospitali ya Muelmed, iliyopo mjini Pretoria, Afrika Kusini na Daktari bingwa wa tiba za michezo na za kawaida aliyebaini Idd amechanika misuli miwili ya paja na Mbaraka anasumbuliwa na Ngiri (Hernia).
  Mbaraka Yussuf anatarajiwa kuwa nje ya Uwanja kwa wiki tatu baada ya matibabu ya Ngiri aliyofanyiwa Afrika Kusini

  “Kwa hiyo Shaaban Idd alipatiwa matibabu katika Hospitali hiyo ya katika Hospitali ya Muelmed na atatakiwa kupumzika kwa muda wa wiki tatu na baada ya hapo ataanza mazoezi madogo madogo na kuweza kurejea kwenye ushindani,” alisema na kuongeza kuhusu Mbaraka.
  “Katika sehemu fulani ya hiyo Ngiri, kulikuwa kuna ukosefu wa damu au kwa kitaalamu tunaita Strangulation (inasumbua), kwa hiyo ilibidi afanyiwe operesheni na baada ya kufanyiwa operesheni alikaa hospitali siku nne kabla ya kurejea nchini,”.
  Tayari Azam FC imeanza maandalizi ya msimu mpya na kwa mujibu wa Mwankemwa, wachezaji wengine wote wapo vizuri na wanaendelea na mazoezi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Wakati Mbaraka ni mchezaji mpya kabisa, aliyesajiliwa dirisha hili kutoka Kagera Sugar ya Bukoba, Shaaban Iddi ni chipukizi aliyepandishwa kutoka timu ya vijana ya Azam FC msimu uliopita
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBARAKA YUSSUF, SHAABAN IDDI NJE WIKI TATU AZAM Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top