• HABARI MPYA

    Friday, July 28, 2017

    HATIMAYE TIBOROHA AFANIKIWA KUMUUZA MSUVA MOROCCO

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KATIBU wa zamani wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha ndiye mtu aliye nyuma ya dili ya winga Simon Msuva kujiunga na klabu ya Difaa Hassani El-Jadida ya Ligi Kuu ya Morocco.
    Tiboroha anaonekana kwenye picha za kusaini mkataba na kutambulishwa kwa Msuva Difaa Hassani El-Jadida leo nchini Morocco – kama mtu ambaye aliyemsimamia mchezaji huyo.
    Na kwa sababu za wazi kabisa, hakuna ubishi Tiboroha ndiye aliyefanya mapatano yote kwa niaba ya Msuva na bila shaka ndiye anayesimama kama Meneja wake, ingawa hilo halikuwahi kuwekwa wazi na upande wowote.
    Dk. Jonas Tiboroha (kulia) akiwa ameshika kwa pamoja na Simon Msuva jezi ya Difaa El Jadida wakati wa makabidhiano leo nchini Morocco
    Dk. Jonas Tiboroha (kulia) akimshuhudia Simon Msuva wakati wa kusaini mkataba huo

    Difaa imepandisha picha kibao katika ukurasa wake wa Facebook zikimuonyesha Msuva akiwa na Tiboroha kuanzia anasaini, anakabidhiwa jezi hadi anatambulishwa kwenye mkutano na Waandishi wa Habari.
    Hata hivyo, si Msuva wala Difaa aliyesema ni mkataba wa miaka mingapi, mchezaji atakuwa analipwa kiasi gani na klabu yake wala Yanga imepata kiasi gani.  
    Ingawa mapema tu habari zisizo za uhakika, zilisema Difaa ambayo tayari imekwishamchukua Mtanzania mwingine, winga pia Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Azam FC ya Dar es Salaam pia, itailipa Yanga dola za Kimarekani 150,000 tu kwa kuwa Msuva alikuwa amebakiza miezi tisa katika mkataba wake.
    Simon Msuva akiwa mwenye furaha baada ya kusaini mkataba na kukab idhiwa jezi
    Msuva alijiunga na Yanga SC mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro na awali ya hapo alipitia akademi ya Azam baada ya kuibuliwa na iliyokuwa taasisi ya Pangollin ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye sasa ni Katibu wa Yanga, klabu aliyoichezea na kuifundisha awali. 
    Baada ya kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mfungaji bora mara mbili – bila shaka sasa ni wakati mwafaka kwa Msuva kwenda kutafuta changamoto mpya nje ya nchi. 
    Timu hiyo yenye maskani yake mji wa El Jadida ikiwa inatumia Uwanja wa El Abdi inataka kuwatumia mawinga wa Tanzania kujaribu kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Morocco, inayojulikana kama Botola, moja ya Ligi bora kabisa barani Afrika.
    Simon Msuva anamkuta Ramadhani Singano 'Messi' tayari amekwishakuwa mwenyeji Difaa El Jadida 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATIMAYE TIBOROHA AFANIKIWA KUMUUZA MSUVA MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top