• HABARI MPYA

    Monday, July 31, 2017

    FIFA YABARIKI UCHAGUZI TFF UENDELEE, NGOMA KUPIGWA ST GASPER

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA) limeridhia mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) uendelee na kama ulivyopangwa utafanyika Agosti 12 kwenye ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma.
    Hatua hiyo inafuatia Meneja Miradi ya Maendeleo wa FIFA kwa Afrika, Mzimbabwe Solomon Mudege kuwa nchini kwa siku ya Jumamosi kwa ajili ya kufuatilia kinachoendela kwenye sokaa ya Tanzania.
    Mudege alizungumza na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Yussuph Singo pamoja na Kamati ya Utendaji wa TFF.
    FIFA imebariki uchaguzi wa TFF uendelee bila Jamal Malinzi (katikati)
    Mara baada ya Mudege kupata maelezo ya kuridhisha kutoka kwa wanafamilia hao wa mpira wa miguu ambao baadhi yao alikutaa nao mmoja baada ya mwingine, alibariki mchakato wa uchaguzi uendelee na Kamati ya Utendaji imetangaza kuwa utafanyika Ukumbi wa St. Gasper mjini Dodoma.
    Ujio wa FIFA unafuatia viongozi wakuu wawili wa TFF, Rais Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa kuwekwa rumande tangu Juni 29 kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. 
    Malinzi, Mwesigwa pamoja na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
    Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
    Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguruma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
    Lakini kwa mwenendo wa kesi, Malinzi ndiyo kama amekwishaaga TFF, kwani uchaguzi unatarajiwa kufanyika Agosti 12 mjini Dodoma naye hajashiriki usaili wa wagombea, hivyo haruhusiwi tena kugombea.  
    Karia naye yupo hatarini kuenguliwa katika uchaguzi baada ya kuitwa Idara ya Uhamiaji ya Taifa kuthibitisha uraia wake, akidaiwa kuwa ni raia wa Somalia. 
    Katika hatua nyingine, Kamati ya Utendaji imeridhishwa na maandalizi ya Mkutano Mkuu ujao wa TFF ambako pamoja na mambo mengine utakuwa na ajenda ya Uchaguzi Mkuu wa shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FIFA YABARIKI UCHAGUZI TFF UENDELEE, NGOMA KUPIGWA ST GASPER Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top