• HABARI MPYA

    Thursday, July 27, 2017

    SIMBA SC KUCHEZA NA ORLANDO PIRATES, BIDVEST AFRIKA KUSINI

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba ya Dar es Salaam inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki katika kambi yake ya Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya, dhidi ya Orlando Pirates na Bidvest Wits za huko wiki ijayo.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba baada ya wiki mbili za mazoezi nchini Afrika Kusini, wiki iayo watacheza mechi mbili dhidi ya Pirates na Bidvest.
    Pamoja na hayo, Manara amekasirishwa na uzushi wa kwamba eti wamefungwa mabao 7-0 na timu ya Royal Eagles katika mchezo wa kirafiki jana kwenye kambi yao ya Afrika Kusini.
    Wachezaji wa Simba wakiwa mazoezini katika kambi yao ya Afrika Kusini kujiandaa na msimu mpya

    “Kwa masikitiko makubwa tunakanusha taarifa potofu zinazosambaa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kuwa (Simba) imecheza mechi ya kirafiki nchini Afrika kusini na kupoteza mchezo huo. Uzushi huo unasema Simba imefungwa mchezo huo kwa jumla ya goli 7-0, na timu ya daraja la kwanza ya nchini humo, Royal Eagles,” amesema Manara. 
    “Kiukweli Simba haina rekodi za hovyo kama hizo kokote inapocheza duniani na haijawahi kufungwa na klabu yoyote idadi ya magoli kama hayo, kama zilivyo klabu nyingine nchini, hususan klabu ambayo mashabiki wake ndiyo wanaozusha upuuzi huo,”. 
    “Dunia ya leo ni ya Teknolojia na ingekuwa ni kweli, hakuna Mtanzania ambaye asingeiona hii taarifa kutoka kwenye mitandao au vyombo vya habari vya Afrika kusini. Tunapenda Umma wa Watanzania utambue kwa siku zote tulizokuwa huko, programu ya benchi la ufundi, ilijikita katika kuitengeneza miili ya wachezaji kistamina,”amesema Manara. 
    “Wiki ijayo Timu yetu inatarajiwa kucheza mechi mbili na klabu za Orlando Pirates na Bidverst za nchini humo, kabla ya kurejea tarehe tano mwezi ujao teyari kwa mchezo wetu wa SIMBA DAY utakaopigwa tarehe nane mwezi ujao,”amesema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUCHEZA NA ORLANDO PIRATES, BIDVEST AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top