• HABARI MPYA

  Saturday, July 15, 2017

  STARS YAANZA VIBAYA MBIO ZA CHAN 2018 KENYA

  Na Rehema Lucas, MWANZA
  TANZANIA imeanza vibaya kampeni za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya mtoano.
  Matokeo hayo yanamaanisha Taifa Stars italazimika kwenda kushinda ugenini mjini Kigali Julai 22 ili kusonga mbele katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchini Kenya, ambako itamenyana na mshindi kati ya Sudan Kusini na Uganda zilizotoa sare ya 0-0 pia jana mjini Juba.
  Katika mchezo wa leo uliofanyika Uwanja ‘mbaya’ eneo la kuchezea, CCM Kirumba mjini Mwanza, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika timu hizo zikiwa tayari zimefungana mabao hayo, Rwanda wakitangulia kabla ya wenyeji kuchomoa. 
  Nahodha wa Tanzania, Himid Mao akiwa ameshika mpira kabla ya kupiga penalti ya bao la kusawazisha 
  Beki wa Taifa Stars, Gardiel Michael (kulia) akijivuta kupiga mpira mbele ya wachezaji wa Rwanda

  Dominique Savio Nshuti alianza kuifungia Amavubi dakika ya Dk 17 akiitelezea krosi ya Emmanuel Imanishimwe kumtungua kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Aishi Salum Manula anayehamia Simba SC kutoka Azam, zote za Dar es Salaam.
  Rwanda walitumia mwanya wa Tanzania kucheza pungufu ya wachezaji wawili kwa zaidi ya dakika moja kutokana na beki Shomari Kapombe kuwa nje baada ya kutolewa kwa machela kufuatia kuumia na winga Shiza Kichuya kuwa chini akiugulia maumivu kufanya shambulizi la haraka kupata bao lao. 
  Kapombe aliumia tangu dakika ya 13 baada ya kuchezewa rafu na Mico Justin, lakini pamoja kulazimisha kuendela kucheza, akashindwa na kutolewa kwa machela dakika ya 16.
  Hata hivyo, benchi la Ufundi la Stars chini ya kocha Salum Shaaban Mayanga likachelewa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Kapombe hadi Rwanda wakaitumia kupata bao la kuongoza ndipo akaingizwa Boniphace Maganga dakika ya 18.
  Taifa Stars wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Nahodha, Himid Mao Mkami ‘Ninja’ dakika ya 34 aliyefunga kwa penalti iliyotolewa na refa Alier Michael James kutoka Sudan Kusini, baada ya Rucogoza Aimable kuunawa mpira uliopigwa na beki Gardiel Michael dakika ya 32. Rwanda walipoteza muda kidogo kwa kumzonga refa kabla ya kutulia na kuruhusu adhabu hiyo ipigwe.
  Taifa Stars ikazinduka baada ya kusawazisha bao na kuanza kucheza kwa maelewano, ingawa tatizo likaendelea kuonekana kwenye safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na John Raphael Bocco kuwa dhaifu.  
  Kipindi cha pili, Tanzania waliendeleza mchezo wa kushambulia, lakini tatizo likabaki kuwa lile lile la utumiaji wa nafasi zinazotengenezwa, huku kipa wa Rwanda, Eric ‘Sungura’ Ndayishimiye akiupoozesha mchezo kwa kuchelewesha muda, jambo ambalo lilimponza akaonyeshwa kadi ya njano.
  Mabishano yalitokea uwanjani dakika ya 51, baada ya beki Salim Mbonde wa Taifa Stars kuunawa mpira nje kidogo ya boksi wakati akiokoa, lakini wachezaji wa Rwanda wakasema aliunawia ndani.
  Na refa Alier Michael James akatofautiana na msaidizi wake namba moja, Abdallah Suleiman Gassim, wote wa Sudan Kusini aliyedai awali kweli tukio hilo lilifanyika ndani ya boksi, kabla ya baadaye kukubali ilikuwa nje.
  Mchezo ukageuka kuwa wa kibabe mwishoni mwa kipindi cha pili, kwa wachezaji kuchezeana rafu nyingi, kusukumana kwa vichwa, ikono na vifua achilia mbali maneno makali waliyokuwa waklitoleana uwanjani.
  Na kwa sababu huyo watu wa huduma ya kwanza waliingia mara kwa mara uwanjani kutoa huduma kwa wachezaji walioumia – na pamoja na Ndayishimiye kupoteza muda mara kwa mara, haikushangaza refa kuongeza dakika nane baada ya dakika 90 za kawaida za mchezo kutimia.
  Kikosi cha Tanzania kilikwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco/Stahmili Mbonde dk93, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya.
  Rwanda; Ndayishimiye Eric, Marcel Mubumbyi/Latif Bishira dk63, Bizimana Djihad, Dominique Savio Nshuti/Innocent Nshuti dk94, Emmanuel Imanishimwe, Iradukunda Eric, Manzi Thierry, Mico Juastin/Kayumba Soter dk81, Yannick Mukunzi, Nsabimane Aimable na Rucogoza Aimable. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: STARS YAANZA VIBAYA MBIO ZA CHAN 2018 KENYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top