• HABARI MPYA

    Sunday, July 16, 2017

    SIMBA SC WAENDA KUWEKA KAMBI AFRIKA KUSINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba SC inatarajiwa kuondoka nchini kesho Alfajiri kwenda nchini Afrika Kusini kwa ziara ya wiki mbili ya kujiandaa na msimu mpya wa 2017/2018.
    Taarifa ya Simba SC leo, imesema kwamba wachezaji waliokuwa mjini Mwanza na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi y Rwanda kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN mwakani nchini Kenya hawataondoka kesho.
    Imeelezwa wachezaji hao watabaki kwenye kambi ya Taifa Stars hadi baada ya mchezo wa marudiano Julai 22 mjini Kigali, Rwanda na baada ya hapo ndipo watasafiri kwenda Johannesrburg.
    Mshambuliaji mpya, John Bocco atajiunga na timu baada ya mchezo wa marudiano na Rwanda Julai 22 mjini Kigali
    Hao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Salim Mbonde, viungo Muzamil Yassin, Said Ndemla na Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco.
    Ikiwa Afrika Kusini pamoja na mazoezi makali ya kujiandaa na msimu mpya, Simba inayofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog itacheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu za Ligi Kuu nchini humo.
    Simba itarejea Dar es Salaam siku chache kabla ya Tamasha kubwa la kila Mwaka la Simba Day, lililopangwa kufanyika kama kawaida Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Siku hiyo Simba itatambulisha kikosi chake kamili cha msimu kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na timu moja kutoka nje, baada ya kutwa iliyopambwa na burudani mbalimbali, ikiwemo zoezi la kuwauzia jezi mpya wapenzi na wanachama wa timu hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAENDA KUWEKA KAMBI AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top