• HABARI MPYA

  Sunday, August 07, 2016

  USAJILI LIGI KUU WAFUNGWA YANGA HAWAJATUMA HATA MCHEZAJI MMOJA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  DIRISHA la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limefungwa Saa 6:00 usiku wa jana na Yanga SC ndiyo timu pekee ambayo imeshindwa kuwasilisha jina hata moja.
  Habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata kutoka TFF zimesema kwamba hadi mtandao wa kimataifa wa usajili (TMS) unafungwa jana usiku, ni Yanga pekee walikuwa hawajatuma jina lolote.
  Timu nyingine zote, zikiwemo zilizopanda Ruvu Shooting, African Lyon na Mbao FC zimetuma usajili wao kwa mujibu wa taratibu na ndani ya muda.
  Hizo ni pamoja na Azam FC, Simba SC, Prisons,
  Mtibwa Sugar, Mwadui FC, Stand United, Mbeya City , Ndanda FC, Majimaji, JKT Ruvu, Kagera Sugar na Toto Africans.
  Watashiriki Ligi gani msimu ujao?

  Alipoulizwa na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jioni hii, Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa alikiri kwamba Yanga na Coastal Union ya Daraja la Kwanza hazijatuma usajili.
  “Mpaka sasa, taarifa tulizonazo ni kwamba, Yanga na Coastal hawajatuma usajili wao hadi TMS inafungwa,”alisema.
  Na akasema kwamba kwa mujibu wa kanuni, timu ambayo inashindwa kutuma usajili wake TMS, moja kwa moja inakuwa imeondolewa kwenye ligi.
  “Zaidi ya hapo, timu hiyo inapaswa kuandaa utetezi wa kushindwa kufanya hivyo na kuuwasilisha TFF, sasa sisi TFF ndiyo tunaupeleka FIFA kuwaomba watufungulie TMS tuingiza usajili wa hiyo timu,”.
  “Na huo utetezi inabidi ukubaliwe na FIFA ndiyo dirisha lifunguliwe, ukikataliwa hiyo timu inateremka hadi daraja ambalo halimo kwenye usajilli wa mfumo wa TMS, ambalo huku kwetu ni la tatu nadhani,”alisema Mwesigwa.
  Katibu huyo amesema kwamba kumekuwa na uzembe kwa Yanga katika mambo mengi na mara kadhaa TFF imekuwa ikiwasaidia, lakini jana ilishindikana.
  “Yanga ni timu pekee ambayo haikutuma mwakilishi kwenye mafunzo ya TMS (mfumo wa usajili wa mtandao), na kama utakumbuka hawakutuma mtu hata kwenye semina elekezi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Cairo,”alisema.
  Mwesigwa alisema mwaka jana pia TFF ilichelewa kukamilisha usajili, ikaomba FIFA iwafungulie dirisha baada ya ufafanuzi mzito, lakini bado walitozwa faini.
  “Kwa hili la sasa sijui kwa kweli. Tuombe Mungu tu FIFA watuelewe, vinginevyo, Yanga sijui itakuwaje,”alisema.
  Mara mbili BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imemtafuta kwenye simu Katibu wa Yanga, Baraka Deusdedit, lakini hakupokea simu yake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: USAJILI LIGI KUU WAFUNGWA YANGA HAWAJATUMA HATA MCHEZAJI MMOJA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top