• HABARI MPYA

  Friday, August 19, 2016

  KIINGILIO POA SERENGETI BOYS NA AFRIKA KUSINI BUKU MBILI CHAMAZI JUMAPILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIINGILIO cha chini katika mchezo wa marudiano Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za Afrika mwakani Madagascar kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, baina ya wenyeji Tanzania ‘Serengeti Boys’ na Afrika Kusini ‘Amajimbos’ kitakuwa ni Sh. 2,000.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba katika mchezo huo utakaoanza Saa 9.00 Alasiri Jumapili ya Agosti 21 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam, kiingilio cha juu katika eneo la VIP kitakuwa ni Sh 5,000.
  Na Lucas amesema mechi hiyo itachezeshwa na Mwamuzi Noiret Jim Bacari wa Comoro atakayesaidiwa na Mmadi Faissoil na Said Omar Chebli wakati mezani atakuwa Ali Mohamed Adelaid huku Kamishna wa mchezo huo atatoka Somalia ambaye anaitwa Amir Abdi Hassan.
  Katika mchezo wa kwanza Jumamosi ya Agosti 6, Serengeti ililazimisha sare ya 1-1 na Afrika Kusini Uwanja wa Dobsonville, Soweto, Johannesburg, mabao yote yakipatikana kipindi cha pili kwa penalti. 
  Afrika Kusini ndio walioanza kupata penalti katika dakika 65 iliyofungwa na Luke Gareth kabla ya Ally Msengi kuisawazishia Serengeti Boys katika dakika ya 70.
  Penalti ya Afrika Kusini ilitokana na mmoja wa mabeki wa Serengeti Boys kumfanyia madhambi Linamandla Mchilizeli wa Amajimbos ndani ya eneo la hatari wakati ile ya Serengeti Boys ilitoakana na beki Luke Donn wa Amajimbos kunawa mpira eneo la hatari. Mwamuzi wa mchezo huo alikuwa, William Koto kutoka Lesotho.
  Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema: “Watanzania wakaribie Chamazi, waje kutushangilia ili tushangilie ushindi kwa pamoja kikosi change kiko vema na ninamshukuru Mungu kwa hilo, akili yangu na akili za wachezaji wangu ni kumuondoa Msauzi (Afrika Kusini).”
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIINGILIO POA SERENGETI BOYS NA AFRIKA KUSINI BUKU MBILI CHAMAZI JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top