• HABARI MPYA

    Friday, August 19, 2016

    KIVUMBI CHA LIGI KUU CHAANZA KESHO, SIMBA NA AZAM WOTE UWANJANI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2016/2016 inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Agosti 20, 2016 kwa michezo mitano huku mabingwa watetezi, Yanga SC ya Dar es Salaam wakisubiri hadi Agosti 31, 2016 kuanza kutetea taji lao.
    Yanga SC inatarajiwa kusafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kucheza na TP Mazembe mchezo wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika Agosti 23, mwaka huu.
    Michezo itakayochezwa kesho ni pamoja na Simba SC itakayoikaribisha Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Taifa, ulioko Chang’ombe Dar es Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni wakati Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji kuanzia Saa 1:00 usiku.
    Kadhalika Stand United ya Shinyanga itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga sawa na Mtibwa Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye Uwanja wa Manungu uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya Mbeya itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC ya huko.
    Wakati ligi ikianza, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Vibali vya kuishi na kufanya kazi vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza inatolewa na TFF. Vilevile tumeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba. Mchezaji hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za malipo.
    TFF imezikumbusha timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya Tanzania toleo la 2016/2017.
    Kila timu inatakiwa kupeleka nakala tatu za mkataba wa mchezaji TFF, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. 
    Baada ya hapo timu na mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji na mchezaji na timu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIVUMBI CHA LIGI KUU CHAANZA KESHO, SIMBA NA AZAM WOTE UWANJANI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top