• HABARI MPYA

  Wednesday, January 13, 2016

  WATAFUKUZA SANA MAKOCHA, MWISHO WA SIKU WATAJIFUKUZA WENYEWE!

  NANI anaweza kujuta juu ya kufukuzwa kwa kocha ambaye alishauri Elias Maguri aachwe ili asajiliwe Abdoulaye Pape N’daw?
  Nani anaweza kujuta kufukuzwa kwa kocha ambaye chini yake timu ilionekana kuteremka kiwango taratibu siku hadi siku?
  Nani anaweza kujuta juu ya kocha ambaye analalamikiwa na wachezaji na wasaidizi wake kwa ukaidi na dharau.
  Sidhani kama yupo mwana Simba atajuta eti kocha Muingereza, Dylan Kerr amefukuzwa – labda tu kujutia muda ambao klabu imepoteza tangu Julai.
  Uamuzi wa kuachana na Kerr umechelewa na hii ni kwa sababu baada ya viongozi wa Simba SC kufukuza fukuza makocha wa maana kwa muda mrefu bila sababu za msingi, ikafika wakati wakajishitukia.

  Naamini viongozi wa Simba SC muda mrefu walikwishajiridhisha ‘wamepotea maboya’ kwa Kerr, lakini wakawa wanajiuliza watamfukuzaje?
  Na wakimfukuza watu watawaelewaje? Wakaacha aendelee hadi pale walipoanza kusikia sikia hata mashabiki wa timu wamemchoka ndipo wakachukua hatua.
  Bila shaka wengi watakuwa wanakumbuka Simba SC waliamua kuangukia kwa Kerr baada ya kushindwa dau la kocha Mserbia, Goran Kopunovic aliyetaka nyongeza ya mshahara na dau la kusaini baada ya kumaliza Mkataba wa awali.
  Lakini viongozi wa Simba SC wakasema hawana uwezo wa kumpa anachotaka Kopunovic aliyeiongoza vizuri timu kwa nusu msimu na wengi wakaridhika naye.
  Na wanakumbuka Kopunovic hakuwa na timu yenye wachezaji wazoefu kama hii ya sasa aliyopewa Kerr, lakini bado Simba SC ilionekana na mwisho wa msimu ilikaribia kuchukua nafasi ya pili katika Ligi Kuu kama si kuzidiwa na Azam FC.
  Viongozi wa Simba SC wakaona kocha  bora kocha, bila kujali ubora wa kocha na wakaamua kuachana na Kopunovic wakaleta Kerr.
  Kiko wapi sasa? Baada ya kuiongoza timu katika mechi 30 za mashindano yote tangu atue Julai kuchukua akishinda 19, kufungwa tano na sare sita Kerr anatupiwa virago.
  Na Kerr anafukuzwa baada ya Simba SC kutolewa katika Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Jumapili, jambo ambalo limemfanya apoteze imani mbele ya uongozi.
  Kerr anatuhumiwa kwa kushindwa kuifanya Simba SC icheze vizuri na uongozi unaamini kiwango cha timu kimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutoka alivyoikuta Julai mwaka jana ilipoachwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
  Aidha, anashutumiwa kwa ushauri wake mbaya kwa uongozi uliosababisha wachezaji kadhaa wazuri akiwemo Elias Maguri wakaachwa na wakasajiliwa wachezaji wa kiwango cha chini kama Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw aliyeachwa Desemba.
  Lakini pia, Kerr anatuhumiwa kwa ukaidi na kutosikiliza ushauri wa watu anaofanya kazi na kwamaba alifikia hadi kumtolea maneno ya kifedhuli, kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa.
  Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na Wasaidizi wake jambo ambalo lilisababisha aliyekuwa Kocha Msaidizi, Suleiman Matola akaondoka na hata kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili (physic), Mserbia Dusan Momcilovic.
  Lakini pia Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya wachezaji, jambo ambalo linapunguza ufanisi ndani ya timu.
  Sasa Mganda Jackson Mayanja atakaimu nafasi ya Kerr kuanzia sasa. Tumpe muda Mayanja, amefundisha Kagera Sugar akisaidiana na Mlage Kabange kwa muda mrefu kabla ya kwenda Coastal Union msimu huu, ambako hakufanya vizuri.
  Mpira hauchezwi chumbani, miezi miwili tu tutajua kama SImba ipo kwenye mikono salama au namna gani. Ila Rais was Simba SC, Evans Aveva na Mwenyekiti wake wa Usajili, Zacharia Hans Poppe kuanzia sasa wajue bure aghali. 
  Maana yake, hata huyo Mayanja kama wamemchukua kwa sababu ni kocha wa bei nafuu, bila kuzingatia kama ni kocha wa kiwango cha Simba SC, basi hadithi itaendelea kuwa ile ile. 
  Naye atafukuzwa. Na mwisho wa siku viongozi wa Simba SC watajifukuza wenyewe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WATAFUKUZA SANA MAKOCHA, MWISHO WA SIKU WATAJIFUKUZA WENYEWE! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top