• HABARI MPYA

    Tuesday, January 12, 2016

    WAPINZANI WA YANGA SC KOMBE LA SHIRIKISHO WAKIONA CHA MOTO TFF

    WAPINZANI wa Yanga SC katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) la Azam Sports HD, Friends Rangers ya Dar es Salaam imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wa timu yake kutoa kashfa na lugha za matusi wakati wa mechi ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes dhidi ya Kiluvya United iliyofanyika Novemba 8, 2015 kwenye Uwanja wa Kaume, Dar es Salaam.
    Rangers pia imetakiwa kulipa kibendera cha kona pamoja ubao wa matangazo wa geti la kuingilia ndani kwenye Uwanja wa Karume, ambavyo vilivunjwa na washabiki wa timu hiyo mara baada ya mechi hiyo.
    Wachezaji wa Friends Rangers wakishangilia katika moja ya mechi zao

    Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi, ambayo pia imeipa Polisi Dodoma ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Mji Mkuu FC kumchezesha mchezaji Peter Ngowi aliyekuwa na kadi tatu za njano kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes iliyochezwa Desemba 26, 2015 mjini Dodoma.
    Uamuzi huo umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 37(4) na 14(37) ya Ligi Daraja la Kwanza. Mji Mkuu FC ilikuwa imeshinda mabao 2-1 katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Mgambo mjini Mpwapwa.
    Kamishna wa mechi ya Ligi ya Daraja la Kwanza ya StarTimes kati ya Polisi Tabora na Panone FC ya Moshi, Shabani Funyenge amesimamishwa kutokana na ripoti yake ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kuwa na upungufu.
    Mtunza vifaa wa timu ya Kimondo, Emily Nehemia, Meneja wa timu ya Polisi Tabora, Idd Kibwana, Kiongozi wa Panone FC, Said watafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutokana na kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes.
    Mji Mkuu FC imepigwa faini ya sh. 100,000 (laki moja) kwa kutohudhuria kikao cha awali cha maandalizi ya mechi (pre match meeting) katika mchezo kati yao na Polisi Dar es Salaam uliochezwa Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Kwanza.
    Klabu za Polisi Tabora na Panone FC kila moja imepigwa faini ya sh. 1,000,000 (milioni moja) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) kugombania kuingia uwanjani kupitia mlango wa VIP badala ya ule wa kawaida kwenye mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes iliyochezwa Januari 2, 2016 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
    Wachezaji Ally Mwanyiro wa Rhino Rangers na Hamisi Shaban wa Lipuli wamepigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kupiga wachezaji wa timu pinzani wakati wa mechi zao za Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes kinyume na Kanuni ya 37(3) ya Ligi hiyo.
    Pia Polisi Mara imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya mshabiki wao kuingia uwanjani na kumvamia mwamuzi kwa madai maamuzi yake hayakuwa sahihi wakati wa mechi yao ya Ligi Daraja la Kwanza ya StarTimes dhidi ya Mbao FC iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAPINZANI WA YANGA SC KOMBE LA SHIRIKISHO WAKIONA CHA MOTO TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top