• HABARI MPYA

  Tuesday, January 12, 2016

  SIMBA SC YATANGAZA RASMI KUMTIMUA KERR NA BENCHI LAKE LOTE, MAYANJA KOCHA MKUU WA MUDA

  REKODI YA DYLAN KERR SIMBA SC;
  Jumla ya Mechi; 30
  Mechi alizoshinda; 19
  Mechi alizofungwa; 5
  Mechi alizotoa sare; 6
  MATOKEO YA MECHI ZA SIMBA SC CHINI KERR;
  Simba SC 2-1 Zanzibar Kombaini (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 4-0 Black Sailor (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 2-0 Polisi (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 3-0 Jang’ombe Boys (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 3-2 KMKM (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 1-0 SC Villa (KIrafiki Simba Day)
  Simba SC 2-1 URA (Kirafiki, Dar es Salaam)
  Simba SC 0-0 Mwadui FC (Kirafiki, Dar es Salaam)
  Simba SC 0-2 JKU (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 3-1 JKU (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 0-0 KVZ (KIrafiki Zanzibar)
  Simba SC 1-0 African Sports (Ligi Kuu Mkwakwani)
  Simba SC 2-0 JKT Mgambo (Ligi Kuu Tanga)
  Simba SC 3-1 Kagera Sugar (Ligi Kuu Taifa)
  Simba SC 0-2 Yanga SC (Ligi Kuu Taifa)
  Simba SC 1-0 Stand United (Ligi Kuu Taifa)
  Simba SC 1-0 Mbeya City (Ligi Kuu Mbeya)
  Simba SC 0-1 Prisons (Ligi Kuu Mbeya)
  Simba SC 1-0 Coastal Union (Ligi Kuu Mbeya)
  Simba SC 6-1 Majimaji FC (Ligi Kuu Taifa)
  Simba SC 5-2 Kimbunga FC (Kirafiki Zanzibar)
  Simba SC 2-2 Azam FC (Ligi Kuu Taifa)
  Simba SC 1-1 Toto Africans (Ligi Kuu Kirumba)
  Simba SC 1-3 Geita Gold Mine (Kirafiki Geita)
  Simba SC 1-1 Mwadui FC (Ligi Kuu Kambarage)
  Simba SC 1-0 Ndanda FC (Ligi Kuu Nangwanda)
  Simba SC 2-2 Jamhuri FC (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-0 URA FC (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 1-0 JKU FC (Kombe la Mapinduzi)
  Simba SC 0-1 Mtibwa Sugar (Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi)
  Dylan Kerr alifanya kitu cha kukumbukwa kabla ya kufukuzwa Simba SC kwa kumsogeza mlemavu mbele atazame vizuri mechi dhidi ya Mtibwa Sugar Jumapili Uwanja wa Amaan, Zanzibar

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imeachana na kocha wake, Mkuu wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr pamoja na kocha wa makipa, Iddi Salim na sasa timu itakuwa chini ya Mganda, Jackson Mayanja.
  Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika kutwa ya leo makao makuu ya klabu, Msimbazi, Dar es Salaam.
  Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo kwamba, klabu imevunja mikataba yake na makocha wote, Kerr na Mkenya Iddi Salim.
  Manara amesema kwa sasa Mayanja atakuwa na timu, huku mchakato wa kumpata kocha mkuu ukiendelea.
  Kerr anaondoka Simba SC baada ya kuiongoza timu katika mechi 30 za mashindano yote tangu atue Julai kuchukua nafasi ya Mserbia, Goran Kopunovic akishinda 19, kufungwa tano na sare sita.
  Na Kerr anafukuzwa baada ya Simba SC kutolewa katika Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Jumapili, jambo ambalo limemfanya apoteze imani mbele ya uongozi.
  Kerr anatuhumiwa kwa kushindwa kuifanya Simba SC icheze vizuri na uongozi unaamini kiwango cha timu kimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutoka alivyoikuta Julai mwaka jana ilipoachwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
  Aidha, anashutumiwa kwa ushauri wake mbaya kwa uongozi uliosababisha wachezaji kadhaa wazuri akiwemo Elias Maguri wakaachwa na wakasajiliwa wachezaji wa kiwango cha chini kama Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw aliyeachwa Desemba.
  Nani kabaki? Benchi la Ufundi lililoanza msimu na Simba SC, kutoka kulia kocha wa makipa Iddi Salim, kocha wa fiziki Dusan Momcilovic, kocha Msaidizi Suleiman Matola na Kocha Mkuu, Dylan Kerr. Wote sasa hawapo.

  Lakini pia, Kerr anatuhumiwa kwa ukaidi na kutosikiliza ushauri wa watu anaofanya kazi na kwamaba alifikia hadi kumtolea maneno ya kifedhuli, kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa.
  Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na Wasaidizi wake jambo ambalo lilisababisha aliyekuwa Kocha Msaidizi, Suleiman Matola akaondoka na hata kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili (physic), Mserbia Dusan Momcilovic.
  Lakini pia Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya wachezaji, jambo ambalo linapunguza ufanisi ndani ya timu.
  Simba SC ilimtangaza Mayanja juzi kuwa Kocha Msaidizi, lakini taarifa za ndani zikabainisha mapema anakwenda kukaimu nafasi ya Kerr, mzaliwa wa Malta, ambaye ataondolewa.
  Kerr, aliyezaliwa Januari 14 mwaka 1967 mjini Valletta alitua Msimbazi Julai mwaka jana na kusaini Mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezewa mmoja mwingine, iwapo angefanya vizuri.
  Beki huyo wa zamani wa kushoto wa Sheffield Wednesday ya England, alitua Simba SC akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Vietnam, Hai Phong aliyojiunga nayo Januari mwaka 2014.
  Lakini Kerr, hakucheza mechi yoyote ya Ligi Kuu England katika miaka yake minne ya kuwa na klabu hiyo ya Hillsborough hivyo akahamia Arcadia Shepherds ya Afrika Kusini mwaka 1988.
  Mwaka mmoja baadaye akarejea England kujiunga na Leeds United, ambako alicheza mechi 13 tu za Ligi Kuu katika miaka yake minne Elland Road kabla ya kutolewa kwa mkopo katika klabu mbili, kwanza Doncaster Rovers alikofunga bao lake la kwanza katika ligi, kisha Blackpool. 
  Katika miezi yake mitatu ya kuwa na Blackpool msimu wa 1991–1992, alifunga moja ya mabao katika ushindi wa 5-2 ugenini dhidi ya Lancashire na mabingwa wa Daraja, Burnley Uwanja wa Bloomfield Road.
  Mganda Jackson Mayanja (kulia) sasa atakuwa kocha wa muda wa Simba SC

  Mwaka 1993, Kerr akahamia Mortimer Common kujiunga na Reading, ambako alicheza mechi nyingi zaidi za ligi katika historia yake (89) na kufunga mabao matano. 
  Alikuwemo kwenye kikosi cha Royals kilichotwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili, na wakati timu hiyo inashika nafasi ya pili katika Daraja la Kwanza msimu uliofuata alikuwepo kikosini.
  Mwaka 1996, Kerr akasaini Kilmarnock ya Scotland, ambako alicheza mechi 61 za ligi Killie katika miaka minne. Mwishoni mwa msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo, alishinda Kombe la Scotland, kabla ya kuumia nyonga na kuwa nje kwa zaidi ya mwaka.
  Kerr akatemwa Kilmarnock, na baada ya mechi moja ya kucheza kwa mkopo Carlisle United akajiunga na Slough Town Oktoba mwaka 2000, kabla ya Septemba mwaka huo kujiunga kwa muda na Kidderminster Harriers, lakini Mkataba wake wa mwezi mmoja ukasitishwa kwa utovu wa nidhamu.
  Akarejea Scotland kujiunga na Hamilton Academical Januari mwaka 2001 na miaka mitatu iliyofuata akacheza timu za Exeter City kwa miezi mitatu, Greenock Morton, Harrogate Town, East Stirlingshire na Hamilton Academical kwa mara nyingine kabla ya kustaafu akiwa na Kilwinning Rangers mwaka 2003.
  Baada ya kutungika daluga zake, Kerr akaenda kufundisha Marekani klabu ya Phoenix, Arizona ambako baada ya kukosa viza ya kuishi nchini humo akalazimika kurejea Scotland, ambako alifanya kazi kama Ofisa Maendeleo wa Argyll na Bute kati ya mwaka 2005 na 2009.
  Septemba mwaka 2009, Kerr akasaini Mkataba wa kuwa kocha Msaidizi wa Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini hadi Juni mwaka 2010 alipohamia Thanda Royal Zulu kama Kocha Msaidizi pia, 2011 akaenda Nathi Lions (Msaidizi), 2012 akaenda Khatoco Khanh Hoa (Msaidizi) na mwaka 2012 akasaini Mkataba wa kuwa kocha wa mazoezi utimamu wa mwili wa timu ya taifa ya Vietnam.
  Mwaka 2013 akahamia Hai Phong kama Kocha Msaidizi pia, kabla ya mwaka 2013 kuwa Kocha Mkuu wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ya Hai Phong na mwaka 2014 akawa kocha Mkuu wa Hai Phong, ambayo aliipa ubingwa wa Taifa wa nchi hiyo, kabla ya kutua Simba SC julai mwaka jana na sasa anafungashiwa virago vyake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YATANGAZA RASMI KUMTIMUA KERR NA BENCHI LAKE LOTE, MAYANJA KOCHA MKUU WA MUDA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top