• HABARI MPYA

  Wednesday, January 13, 2016

  URA BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI 2016, WAICHAKAZA MTIBWA SUGAR 3-1 AMAAN

  ORODHA YA MABINGWA KOMBE LA MAPINDUZI
  Mwaka     Bingwa Mshindi wa Pili
  2007 Yanga SC  Mtibwa Sugar 
  2008 Simba SC  Mtibwa Sugar
  2009 Miembeni          KMKM
  2010 Mtibwa Sugar   Ocean View
  2011 Simba SC   Yanga SC
  2012 Azam FC          Simba SC
  2013  Azam FC    Tusker FC
  2014 KCCA        Simba SC
  2015 Simba SC Mtibwa Sugar
  2016 URA                 Mtibwa Sugar
  Wachezaji wa URA wakisherehekea na Kombe lao baada ya kukabidhiwa Uwanja wa Amaan

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  URA ya Uganda imetwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2016 kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Ushindi huo ambao unakwenda sambamba na kitita cha Sh. Milioni 10, unaifanya URA iwe timu ya pili ya Uganda kutwaa taji hilo, baada ya KCCA mwaka juzi.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mfaume Ali Nassor, hadi mapumziko, URA walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na Julius Ntambi kwa kichwa, akimalizia krosi ya Villa Oromchani kutoka upande wa kushoto.
  URA walikaribia kupata bao la pili dakika ya 37 baada ya Elkannah Nkugwa kupiga nje na kupoteza pasi ya Moor Semakula.
  Kwa ujumla, URA ilitawala mchezo na kuishika Mtibwa Sugar, ambayo safu yake ya ushambuliaji ikiongozwa na Hussein Javu anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC, iliishindwa kupasua ukuta wa timu ya Mamlaka ya Mapato Uganda.
  Kipindi cha pili, Mtibwa Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mecky Mexime ilijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi kusaka bao la kusawazisha, lakini wakasahau kuongeza umakini wa kujilinda, hivyo kuwapa fursa URA kupata mabao mawili zaidi.
  Peter Lwasa aliyeingia dakika ya 53 kuchukua nafasi ya Villa Oromchani, aliifungia URA mabao mawili ndani ya dakika tatu – kwanza dakika ya 85 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki Dickson Daud na lingine dakika ya 88 akimalizia pasi ya Julius Ntambi.
  Jaffar Salum aliyeingia kuchukua nafasi ya Hussein Javu mwishoni mwa kipindi cha pili, aliifungia bao la kufutia machozi Mtibwa Sugar dakika ya 90, baada ya kuunasa mpira wakati kipa Brian Bwette anajaribu kumpiga chenga.
  Pamoja na kutwaa ubingwa, URA pia imetoa mfungaji bora, ambaye ni Peter Lwasa aliyemaliza na mabao matatu, akifuatiwa na Villa Oramchani wa URA pia, mabao mawili sawa na Awadh Juma wa Simba SC, Donald Ngoma wa Yanga SC, Mohammed Abdallah wa JKU na Kipre Tchetche wa Azam FC.
  Mtibwa Sugar wamepatiwa Sh. Milioni 5 kwa kushika nafasi ya pili. 
  Kikosi cha URA FC kilikuwa; Brian Bwete, Simon Massa, Alan Munaaba, Jimmy Kulaba, Sam Senkoom, Oscar Agaba, Julius Ntambi, Said Kyeyune, Moor Semakula/Shafiq Kagimu dk48, Villa Oramuchani/Peter Lwasa dk53 na Elkannah Nkugwa/Sam Sekito dk74.
  Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Ally Shomary, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Dickson Daudi, Salim Mbonde, Shaaban Nditi, Mohammed Ibrahim, Muzammil Yassin, Hussein Javu/Jaffar Salum dk81, Ibrahim Rajab ‘Jeba’ na Shiza Kichuya/Said Bahanuzi dk69.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: URA BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI 2016, WAICHAKAZA MTIBWA SUGAR 3-1 AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top