• HABARI MPYA

  Tuesday, January 12, 2016

  TAMATI YA KERR SIMBA SC YANUKIA, AITWA KWENYE KIKAO KUJIBU TUHUMA NZITO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Muingereza Dylan Kerr anaweza kuondolewa kazini iwapo hatakuwa na hoja za utetezi za kuiridhisha Kamati ya Utendaji ya klabu.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata kutoka ndani ya Simba SC zinasema kwamba baada ya timu kutolewa hatua ya Nusu Fainali Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Jumapili, Kerr amepoteza imani mbele ya uongozi.
  Na Kamati ya Utendaji, chini ya Rais, Evans Elieza Aveva inatarajiwa kuumuhoji masuala mbalimbali Kerr katika kikao kinachotarajiwa kufanyika Jumanne asubuhi Dar es Salaam.
  Wazi iwapo Kerr hatakuwa na hoja za maana za utetezi juu ya shutuma na tuhuma mbalimbali zinazomkabili juu ya mwenendo wa timu, basi atakuwa amehitimisha siku zake za kuwa kocha wa Simba SC.
  Kerr anatuhumiwa kwa kushindwa kuifanya Simba SC icheze vizuri na uongozi unaamini kiwango cha timu kimeporomoka kwa kiasi kikubwa kutoka alivyoikuta Julai mwaka jana ilipoachwa na Mserbia, Goran Kopunovic.
  Aidha, anashutumiwa kwa ushauri wake mbaya kwa uongozi uliosababisha wachezaji kadhaa wazuri akiwemo Elias Maguri wakaachwa na wakasajiliwa wachezaji wa kiwango cha chini kama Msenegali, Abdoulaye Pape N’daw aliyeachwa Desemba.
  Dylan Kerr Jumapili alishindwa kuinusuru Simba SC kutolewa na Mtibwa Sugar katika Kombe la Mapinduzi 

  Lakini pia, Kerr anatuhumiwa kwa ukaidi na kutosikiliza ushauri wa watu anaofanya kazi na kwamaba alifikia hadi kumtolea maneno ya kifedhuli, kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa.
  Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na Wasaidizi wake jambo ambalo lilisababisha aliyekuwa Kocha Msaidizi, Suleiman Matola akaondoka na hata kocha wa mazoezi ya utimamu wa mwili (physic), Mserbia Dusan Momcilovic.
  Lakini pia Kerr anatuhumiwa kutokuwa na maelewano mazuri na baadhi ya wachezaji, jambo ambalo linapunguza ufanisi ndani ya timu.
  Tuhuma ni nyingi ambazo atasomewa Kerr asubuhi ya Jumanne na kwa sababu hiyo – uwezekano wa kubaki Msimbazi ni mdogo, haswa ikizingatiwa tayari klabu imekwishaingia Mkataba na kocha Mganda, Jackson Mayanja.
  Simba SC ilimtangaza Mayanja juzi kuwa Kocha Msaidizi, lakini taarifa za ndani zikabainisha mapema anakwenda kukaimu nafasi ya Kerr, mzaliwa wa Malta, ambaye ataondolewa.
  Kerr, aliyezaliwa Januari 14 mwaka 1967 mjini Valletta alitua Msimbazi Julai mwaka jana na kusaini Mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongezewa mmoja mwingine, iwapo angefanya vizuri.
  Beki huyo wa zamani wa kushoto wa Sheffield Wednesday ya England, alitua Simba SC akitokea klabu ya Ligi Kuu ya Vietnam, Hai Phong aliyojiunga nayo Januari mwaka 2014.
  Lakini Kerr, hakucheza mechi yoyote ya Ligi Kuu England katika miaka yake minne ya kuwa na klabu hiyo ya Hillsborough hivyo akahamia Arcadia Shepherds ya Afrika Kusini mwaka 1988.
  Mwaka mmoja baadaye akarejea England kujiunga na Leeds United, ambako alicheza mechi 13 tu za Ligi Kuu katika miaka yake minne Elland Road kabla ya kutolewa kwa mkopo katika klabu mbili, kwanza Doncaster Rovers alikofunga bao lake la kwanza katika ligi, kisha Blackpool. 
  Katika miezi yake mitatu ya kuwa na Blackpool msimu wa 1991–1992, alifunga moja ya mabao katika ushindi wa 5-2 ugenini dhidi ya Lancashire na mabingwa wa Daraja, Burnley Uwanja wa Bloomfield Road.
  Mwaka 1993, Kerr akahamia Mortimer Common kujiunga na Reading, ambako alicheza mechi nyingi zaidi za ligi katika historia yake (89) na kufunga mabao matano. 
  Alikuwemo kwenye kikosi cha Royals kilichotwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Pili, na wakati timu hiyo inashika nafasi ya pili katika Daraja la Kwanza msimu uliofuata alikuwepo kikosini.
  Mwaka 1996, Kerr akasaini Kilmarnock ya Scotland, ambako alicheza mechi 61 za ligi Killie katika miaka minne. Mwishoni mwa msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo, alishinda Kombe la Scotland, kabla ya kuumia nyonga na kuwa nje kwa zaidi ya mwaka.
  Kerr akatemwa Kilmarnock, na baada ya mechi moja ya kucheza kwa mkopo Carlisle United akajiunga na Slough Town Oktoba mwaka 2000, kabla ya Septemba mwaka huo kujiunga kwa muda na Kidderminster Harriers, lakini Mkataba wake wa mwezi mmoja ukasitishwa kwa utovu wa nidhamu.
  Akarejea Scotland kujiunga na Hamilton Academical Januari mwaka 2001 na miaka mitatu iliyofuata akacheza timu za Exeter City kwa miezi mitatu, Greenock Morton, Harrogate Town, East Stirlingshire na Hamilton Academical kwa mara nyingine kabla ya kustaafu akiwa na Kilwinning Rangers mwaka 2003.
  Baada ya kutungika daluga zake, Kerr akaenda kufundisha Marekani klabu ya Phoenix, Arizona ambako baada ya kukosa viza ya kuishi nchini humo akalazimika kurejea Scotland, ambako alifanya kazi kama Ofisa Maendeleo wa Argyll na Bute kati ya mwaka 2005 na 2009.
  Septemba mwaka 2009, Kerr akasaini Mkataba wa kuwa kocha Msaidizi wa Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini hadi Juni mwaka 2010 alipohamia Thanda Royal Zulu kama Kocha Msaidizi pia, 2011 akaenda Nathi Lions (Msaidizi), 2012 akaenda Khatoco Khanh Hoa (Msaidizi) na mwaka 2012 akasaini Mkataba wa kuwa kocha wa mazoezi utimamu wa mwili wa timu ya taifa ya Vietnam.
  Mwaka 2013 akahamia Hai Phong kama Kocha Msaidizi pia, kabla ya mwaka 2013 kuwa Kocha Mkuu wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ya Hai Phong na mwaka 2014 akawa kocha Mkuu wa Hai Phong, ambayo aliipa ubingwa wa Taifa wa nchi hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMATI YA KERR SIMBA SC YANUKIA, AITWA KWENYE KIKAO KUJIBU TUHUMA NZITO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top