• HABARI MPYA

  Wednesday, July 19, 2017

  YANGA YAMTIA KITANZI KAMUSOKO MIAKA MIWILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIUNGO Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko leo amesaini mkataba mpya wa miaka miwili kuendelea kuichezea Yanga baada ya mavutano na uongozi kwa takriban mwezi mmoja.
  Baada ya kusaini mkataba huo mpya utakaomfanya adumu Jangwani hadi Julai 2019, Kamusoko atajiunga na wenzake kwa mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya.
  Mchezaji huyo mtaalamu wa kugawa pasi, alisajiliwa Yanga SC mwaka 2015 kutoka FC Platinums ya kwao, Zimbabwe pamoja na mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye naye tayari ameongeza mkataba Jangwani. 
  Wachezaji 16 tayari wapo mazoezini Yanga SC kwa sasa wakiendelea na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.
  Hao ni pamoja wapya wanne, kipa Mcameroon, Youthe Rostand aliyesajiliwa kutoka African Lyon, beki Abdallah Hajji ‘Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe, kiungo Pius Buswita kutoka Mbao FC na mshambuliaji Ibrahim Ajib kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
  Wengine ni mabeki, Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Pato Ngonyani, Mwinyi Hajji Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, viungo Geoffrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma Makapu, Emmanuel Martin, Yussuf Mhilu, Obrey Chirwa na mshambuliaji Amissi Tambwe.
  Wachezaji ambao hawapo ni pamoja na majeruhi watatu, kipa Benno Kakolanya, kiungo Deus Kaseke na Ngoma ambaye anatarajiwa kurejea wakati wowote kutoka Afrika Kusini alipokwenda kwa matibabu.
  Beki Hassan Kessy na winga Simon Msuva wapo na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambacho leo kimekwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Rwanda mwisjoni mwa wiki kuwania tiketi ya CHAN 2018 nchini Kenya, baada ya sare ya 1-1 Jumamosi mjini Mwanza.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAMTIA KITANZI KAMUSOKO MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top