• HABARI MPYA

    Wednesday, July 19, 2017

    ERASTO NYONI AIGEUKA YANGA, ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba imewazidi ujanja mahasimu, Yanga baada ya kufanikiwa kukamilisha usajili wa mchezaji kiraka, Erasto Edward Nyoni kutoka Azam FC kama mchezaji huru.
    Nyoni leo amesaini mkataba wa miaka miwili pamoja na kipa Said Mohammed Mduda kabla ya kwenda Rwanda na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa marudiano na Amavubi Jumamosi mjini Kigali kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
    Habari za kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi, Nyoni kwenda Simba ni pigo kwa Yanga, ambao walikuwa wamekwishaanza naye mazungumzo.
    Erasto Nyoni leo amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba akitokea Azam FC kama mchezaji huru

    Erasto ni mchezaji pekee ambaye alikuwepo timu ya taifa kanzia wakati wa Mbrazil, Marcio Maximo mwaka 2006 na ameendelea kuitwa na kila kocha aliyefuatia kupewa jukumu la kuifundisha timu hiyo kuanzia Wadenmark Jan Borge Poulsen, Kim Poulsen, Mholanzi, Mart Nooij na wazalendo Mkwasa na huyu wa sasa, Salum Mayanga.
    Pamoja na kucheza nafasi za ulinzi, lakini Nyoni ameifungia Stars mabao manne ya kukumbukwa, likiwemo bao pekee katika ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji Burkina Faso, Juni 16, mwaka 2007 mjini Ouagadougou katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2010.
    Na hilo ndilo lilikuwa bao lake la kwanza Taifa Sars kabla ya kufunga tena Juni 10, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao la ushindi, Tanzania ikiilaza 2-1 Gambia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.
    Akafunga bao la kwanza katika sare ya 3-3 na wenyeji Botswana Uwanja wa Molepolole mjini Molepolole, Agosti 15, 2012 kwenye mchezo wa kirafiki, kabla ya Julai 5, mwaka huu kufunga bao la kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikifungwa 4-2 na Zambia waliotoka nyuma kwa 1-0.
    Nyoni ambaye Mei 7, mwaka huu amefikisha miaka 29, amekuwa mchezaji wa Azam FC tangu mwaka 2010 alipojiunga nayo kutoka Vital’O ya Burundi iliyomchukua AFC ya Arusha alikocheza kidogo tu akitokea kituo cha Rollingston cha mjini humo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ERASTO NYONI AIGEUKA YANGA, ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top