• HABARI MPYA

    Sunday, July 02, 2017

    SOKA YA TANZANIA ‘IMETIWA DOA’, TUSUBIRI TUONE MWISHO WAKE

    SOKA ya Tanzania imepigwa ganzi, baada ya viongozi wakuu wa Shirikisho la mchezo huo nchini (TFF) na klabu ya Simba kuwekwa rumande Alhamisi kwa makosa tofauti.  
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa pamoja na Mhasibu wa Shirikisho, Nsiande Isawafo Mwanga walinyimwa dhamana na kupelekwa mahabusu hadi Julai 3, mwaka huu kufuatia kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Hakimu mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Wilbord Mashauri aliwanyima dhamana watatu hao kufuatia mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa utetezi dhidi ya mawakili wa upande wa Serikali.                        
    Katika mashitaka hayo, 25 yamekwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu.
    Kwa upande wa Simba SC, Rais Evans Elieza Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ wako mahabusu hadi Julai 13, mwaka huu baada ya kunyimwa dhamana Alhamisi kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
    Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi siku hiyo na kusomewa mashitaka hayo matano mchana, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
    Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
    Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha pia likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha Barclays baada ya kughushi nyaraka.
    Baada ya kusomewa mashitaka hayo na wakili wa Serikali, Christopher Msigwa, washitakiwa hao walikana mashitaka yote na kupelekwa rumande hadi Julai 13, mwaka huu huku wakinyimwa dhamana.
    Walipandishwa mahakamani baada ya kukamatwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Jumatano kwa uchunguzi juu ya tuhuma hizo.
    Japokuwa bado ni tuhuma na hawajatiwa hatiani, lakini kwa Malinzi na Kaburu athari ya kwanza ni kupoteza haki yao ya kugombea katika uchaguzi wa TFF uliopangwa kuifanyika Agosti 12, mwaka huu Dodoma.
    Hiyo inafuatia wote wawili kutohudhuria usajili, zoezi lililofikia tamati rasmi jana na Kamati ya Uchaguzi ikagawanyika juu ya pendekezo la kuwapitisha moja kwa moja wagombea hao.
    Mwenyekiti, Revocatus Kuuli alikataa kukubaliana na wazo la Wajumbe wenzake wengine wote waliotaka Malinzi apitishwe moja kwa moja kwa sababu aliwasilisha barua ya sababu za kutohudhuria usaili.
    Hilo la uchaguzi si muhimu tena kwa sasa, kwani Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limetuma wajumbe wake kuja kutazama kinachoendelea.
    FIFA inazuia Serikali na vyombo vya dola kuingilia uendeshwaji wa soka, lakini hivi karibuni imeshuhudiwa Shirika la Upepelezi la Marekani (FBI) likisaidia kung’olewa madarakani kwa aliyekuwa Rais wa FIFA, Sepp Blatter kabla ya uchaguzi kumuweka madarakani Gianni Infantino.
    FIFA chini yake Rais wake mpya, Mtaliano Gianni Infantino haitapendezewa na aina yoyote ya ufisadi nani ya soka ya Tanzania, lakini haiwezi kuunga mkono uonevu wowote.
    FIFA ya sasa ni makini, tofauti na ile ya Blatter iliyokuwa ikiendeshwa kwa kukariri tu kwamba vyombo vya dola haviwezi kuingilia uendeshwaji wa soka, hapana.
    Infantino amepitia mgongo wa FBI kuukamata Urais wa FIFA na itakuwa ajabu asiheshimu chombo kingine cha uchunguzi dhidi ya makosa ya jinai kama yaliyomng’oa Blatter kwenye bodi ya soka ya dunia.
    Lakini pia, Infantino hawezi kuwa tayari kuruhusu chuki za aina yoyote, au misimamo isiyozingatia misingi ya haki na sheria iwakandamize watu ndani ya TFF.
    Pamoja na yote, tuhuma hizi ambazo tayari zinafahamika dunia nzima, zimeitia doa soka ya Tanzania. Tusubiri tu tone mwisho wake.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SOKA YA TANZANIA ‘IMETIWA DOA’, TUSUBIRI TUONE MWISHO WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top