• HABARI MPYA

  Saturday, July 01, 2017

  KARIA KAIMU RAIS TFF, FIFA WAJA KUCHUNGUZA KESI YA MALINZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), iliyokutana leo Jumamosi Julai 01, 2017 kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam imempitisha Wallace Karia kuwa Kaimu Rais wa shirikisho.
  Kadhalika, Kamati hiyo ya Utendaji ya TFF, imempitisha Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa TFF.
  Viongozi hao watakaimu nafasi hizo tajwa hadi hapo mahakama itakavyoamua kuhusu kesi zinazowakabili kwa sasa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Mwesigwa Selestine. 
  Kamati ya Utendaji ya TFF, imekutana kwa dharura kwa mujibu wa Ibara ya 35 (1) inayosomwa pamoja na Ibara ya 35 (6) na kufanya uamuzi huo.
  Wallace Karia ameteuliwa kukaimu nafasi ya Umakamu wa Rais wa TFF, wakati huu Jamal Malinzi yuko rumande 

  Malinzi, Mwesigwa kwa pamoja na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga wako rumande baada ya kunyimwa dhamana Alhamisi na wanatarajiwa kufikishwa tena Mahakamani Jumatatu.
  Watatu hao, Alhamisi walisomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
  Hakimu mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, Wilbord Mashauri aliwanyima dhamana watatu hao kufuatia mabishano ya kisheria baina ya mawakili wa utetezi dhidi ya mawakili wa upande wa Serikali.                        
  Katika hatua nyingine, Karia amesema ujumbe wa FIFA unakuja nchini kufuatilia sakata zima la viongozi hao wa TFF kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
  Wakati huo huo:  Uchaguzi ya Chama cha Soka ya Wanawake (TWFA), imetangaza majina ya wagombea 11 waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 5, mwaka huu mkoani Morogoro.
  Majina ambayo yamepitishwa ni Amina Karuma, Rose Kisiwa, Somoe Ng’itu, Theresia Mung’ong’o, Hilda Masanche, Salma Wajeso, Zena Chande, Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmin Soudy na Chichi Mwidege.
  Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mweka Hazina, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KARIA KAIMU RAIS TFF, FIFA WAJA KUCHUNGUZA KESI YA MALINZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top