• HABARI MPYA

    Saturday, July 22, 2017

    SHUGHULI PEVU AMAVUBI NA TAIFA STARS NYAMIRAMBO LEO

    Na Innocent Okama, KIGALI
    TANZANIA wanamenyana na wenyeji, Rwanda leo katika mchezo wa ushindani na upinzani mkali kuwania kusogea hatua ya mwisho ya mtoano wa kupigania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Kenya, michuano inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee.
    Timu hizo zitateremka katika Uwanja wa Kigali, maarufu kama Nyamirambo katika mchezo utakaoanza Saa 9:30 kwa Saa za Rwanda zikitoka kutoa sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Maana yake, Taifa Stars watalazimika kushinda ugenini leo, au kutoa sare ya kuanzia mabao 2-2 ili kusonga mbele, lakini vinginevyo wataishia hatua ya kwanza kabisa ya kuwania fainali za CHAN mwakani. 
    Nahodha Himid Mao alifunga bao la kusawazisha wiki iliyopita Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza

    Kocha wa Amavubi, Antoine Hey amekuwa akimkatisha tamaa kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga kwamba sare ya 1-1 mjini Mwanza tayari ulikuwa ni ushindi kwa Rwanda na leo wanaingia Uwanja Kigali kukamilisha ratiba tu.
    “Tumefanya mazoezi vizuri sana. Hatuna majeruhi na wachezaji wanaonekana kuelekeza fikra zao mno kwenye mchezo, kuliko ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza. Kwa kweli, nafikiri tupo kwenye nafasi nzuri ya kumalizia kazi tuliyoianza Mwanza, hatupo chini ya presha,” amesema Hey.
    “Mechi hii ni maalum mno kwetu na tunatakiwa kuianza vizuri kama tulivyofanya mechi ya kwanza tulipotangulia kufunga sisi, lakini tukaimalizia na walinzi wanane ili kulinda bao letu la ugenini, lakini sifikiri tutarudia mbinu zile zile mbele ya mashabiki wetu nyumbani,”alisema.
    Kwa upande wake, kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga pia anajiamini kwamba watapata matokeo wanayoyahitaji leo mjini Kigali ili kusonga mbele.
    Mayanga alisema wachezaji wake walicheza vizuri katika mchezo wa kwanza licha ya kulazimishwa sare, “Kuwaruhusu Amavubi kufunga bao la mapema lilikuwa kosa kubwa tulilofanya upande wetu. Tulicheza vizuri sana, tulitawala mchezo, tulikuwa na nafasi nyingi za kufunga ili kushinda mchezo, lakini tuliambulia sare tu, matokeo ambayo hatukuyatarajia kabisa. Lengo kubwa ni kuhakikisha tunarakebisha makosa Jumamosi,”alisema.
    Katika mchezo wa kwanza, mchezaji mpya wa AS Kigali, Dominique Savio Nshuti aliifungia Rwanda bao la kuongoza dakika ya 18, kabla ya Nahodha wa Taifa Stars Himid Mao kuisawazishia timu yake kwa penalti dakika ya 35.
    Mshindi wa jumla baina ya Rwanda na Tanzania atamenyana na mshindi kati ya Uganda au Sudan Kusini katika hatua ya mwisho ya mchujo mwezi ujao. 
    Tanzania imecheza mara moja tu fainali za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast ambazo zilikuwa za kwanza kufanyika kihistoria na kutolewa hatua ya makundi tu, wakati Rwanda imeshiriki fainali mbili, mwaka 2011 ilipotolewa hatua ya makundi nchini Sudan na 2016 walipofika Robo Fainali wakiwa wenyeji.
    Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki timu yetu, wabariki wachezaji wetu. Mungu ibariki Tanzania yetu ing’are leo ugenini na kuwapa faraja wananchi wake. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SHUGHULI PEVU AMAVUBI NA TAIFA STARS NYAMIRAMBO LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top