• HABARI MPYA

  Saturday, July 15, 2017

  KILA LA HERI TAIFA STARS, TUNATAKA TIKETI YA CHAN

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  TANZANIA, Taifa Stars leo inaanza kampeni za kuwania tiketi ya pili ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee kwa kumenyana na Rwanda Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Tanzania, Taifa Stars iliyokuwa miongoni mwa nchi nane za kwanza kabisa kucheza fainali za kwanza za michuano hiyo mwaka 2009 nchini Ivory Coast, inaingia kwenye michuano hiyo baada ya wiki moja ikitoka kutwaa Medali ya Shaba katika michuano ya COSAFA Castle nchini Afrika Kusini.
  Kocha Salum Shaaban Mayanga aliweka wachezaji wengi vijana wadogo na wanaocheza nyumbani kwenye kikosi chake kilichoshinda nafasi ya tatu ya michuano hiyo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika baada ya kuifunga Lesotho kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
  Na Stars ambayo katika Nusu Fainali ilitolewa na Zambia kwa kuchapwa mabao 4-2, kikosini ilikuwa ina wachezaji wawili tu wanaocheza nje, Thomas Ulimwengu wa AFC Eskilstuna ya Sweden na Elias Maguri wa Dhofar SC ya Oman, ambao kocha aliwachukua kwenda kuwatazama baada ya kutowaita tangu aanze kazi Machi mwaka huu.
  Lakini Mayanga amepata pigo moja tu, kwani baada ya COSAFA amempoteza beki Abdi Hassan Banda aliyesaini miaka mitatu kujiunga na Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini kutoka Simba SC na kujitoa mapema katika kikosi cha CHAN.
  Uzuri ni kwamba Banda alikwishaanza kumzoesha Mayanga kupanga timu yake bila yeye, kufuatia kukosekana katika mchezo wa Robo Fainali dhidi ya wenyeji Afrika Kusini kwa sababu ya adhabu ya kadi za njano, lakini Taifa Stars ikamudu kuifunga 1-0 Bafana Bafana na kusogea mbele.
  Katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu pia, Banda aliingia dakika za mwishoni kabisa baada ya Mayanga kuwaanzisha pamoja Nurdin Chona wa Prisons ya Mbeya na Salim Mbonde aliyesajiliwa Simba SC kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro dirisha hili na wakacheza vizuri.  
  Sehemu pekee ambayo inatia shaka ni katika safu ya ushambuliaji, kwani katika mechi zote za COSAFA Maguri alikuwa anaanza na wakati mwingine alipangwa pamoja na Ulimwengu, ambao wote leo hawapo.
  Stahmili Mbonde alikuwa anapata muda mfupi wa kucheza kabla ya kuanzishwa kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu – wakati mshambuliaji mwingine, Mbaraka Yussuf aliumia baada ya mechi mbili za mwanzo za Kundi A, tena zote naye akiingia kutokea benchi.
  Mapema tu kocha Mayanga akamuongeza kikosini mshambuliaji aliyeoondoka Azam FC baada ya miaka tisa kuhamia Simba, John Bocco. Aliporejea Dar es Salaam, akawaongeza pia Athanas Mdamu na Kelvin Sabato katika safu hiyo.
  Zaidi ya hapo, Taifa Stars leo inatarajiwa kurudi vile vile kama ilivyokuwa COSAFA, sintofahamu nyingine ikiwa ni langoni, haijulikani nani ataanza kati ya Aishi Salum Manula na Said Mohammed Mduda.
  Manula alidaka mechi zote za COSAFA kabla ya Mduda kuanza katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu na akafanya kazi nzuri kiasi cha kuchaguliwa kipa bora wa mashindano. 
  Kitu kizuri ni rekodi nzuri ya kocha Mayanga kutopoteza mechi ya nyumbani kati ya zote tatu, akishinda mbili 2-0 na Botswana na 2-1 na Burundi kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Lesotho mjini Dar es Salaam.
  Kwa ujumla Mayanga, kocha na mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar amepoteza mechi moja tu tangu achukue nafasi ya mzalendo mwenzake, Charles Boniface Mkwasa Taifa Stars Machi mwaka huu, ambayo ni ya kipigo cha 4-2 kutoka kwa Zambia.
  Zaidi ya hapo ameshinda 2-0 na Botswana na 2-1 na Burundi mechi za kiafiki, 2-0 na Malawi na ushindi wa matuta dhidi ya Lesotho COSAFA, baada ya awali kutoa nao sare ya 0-0 Mamba hao mjini Dar es Salaam mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, 0-0 na Angola na 1-1 na Mauritius kwenye COSAFA.
  Ni matarajio, Taifa Stars itaendelea kuwafurahisha Watanzania na leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza. Kila la heri timu yetu, Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Taifa Stars. Amin. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA STARS, TUNATAKA TIKETI YA CHAN Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top