• HABARI MPYA

    Wednesday, July 19, 2017

    KIPA BORA COSAFA ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeendelea kujiimarisha kwa kumsajili kipa Said Mohammed Mduda kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro.
    Mduda amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Wekundu hao wa Msimbazi, kabla ya kusafiri na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars leo kwenda Rwanda.
    Mduda kwa sasa ni kipa wa pili wa Taifa Stars baada ya Aishi Salum Manula ambaye pia amesajiliwa Simba SC kutoka Azam FC dirisha hili.
    Na Simba imeamua kumsajili Mduda, kipa wa zamani wa Yanga SC baada ya kuteuliwa Kipa Bora wa michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini mwezi uliopita licha ya kudaka mechi moja tu ya kusaka mshindi wa tatu, akimpiku Manula aliyedaka mechi zote tano za awali.
    Said Mohammed amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba kabla ya kusafiri na aifa Stars leo kwenda Rwanda

    Manula alidaka Stars ikishinda 2-0 dhidi ya Malawi, ikitoa sare ya 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius, ikishinda 1-0 dhidi ya Afrika Kusini na katika kipigo cha 4-2 dhidi ya Lesotho, lakini haikumsaidia kuonekana bora mbele ya jopo la wataalamu wa COSAFA.
    Lakini Mduda baada ya kudaka vizuri ndani ya dakika 90 tu dhidi ya Lesotho na kwenda kuiongoza Stars kushinda kwa penalti 4-2 na kushika nafasi ya tatu, amekuwa kipa bora wa mashindano ya 2017.
    Mduda alipangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle kufuatia Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
    Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao, Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
    Kutokana na ushindi huo, Tanzania ilipata dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
    Lakini rejea mwaka 2012 ni Simba SC iliyomponza Mduda kufukuzwa Yanga SC baada ya kumfunga mabao manne ndani ya dakika 45 za kipindi cha pili Mei 6, mwaka huo katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Wekundu hao wa Msimbazi wakishinda 5-0.
    Siku hiyo, Mganda Emmanuel Okwi alifunga mawili dakika ya pili na ya 62, mengine matatu yakifungwa kwa penalti na Felix Sunzu dakika ya 56, Juma Kaseja dakika ya 67 na Patrick Mafisango dakika ya 72.
    Mduda anakwenda kufanya idadi ya makipa watatu Simba baada ya Manula na Emmanuel Mseja aliyesajiliwa kutoka Mbao FC, kufuatia wote wa msimu uliopita Mghana Daniel Agyei na wazalendo Peter Manyika na Dennis Richard kutemwa.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPA BORA COSAFA ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top