• HABARI MPYA

    Wednesday, July 19, 2017

    AZAM FC YAENDA MBEYA KESHO KUIVAA MBEYA CITY JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kinatarajia kuelekea mkoani Mbeya kesho Alhamisi, tayari kabisa kuvaana na wenyeji wao Mbeya City Jumamosi ijayo katika Uwanja wa Sokoine.
    Mchezo huo wa kirafiki ni maalumu kwa ajili ya Mbeya City kutambulisha jezi zao za msimu ujao kwa mashabiki wake.
    Azam FC inautumia mwaliko huo kujiandaa vema kulekea msimu ujao, ambapo mbali na mchezo huo pia itaelekea katika mikoa mingine miwili ya Nyanda za Juu Kusini, Njombe na Iringa kucheza mechi mbili za maandalizi.
    Ikimaliza ziara yake mkoani Mbeya, Azam FC itaelekea mjini Njombe kukipiga na timu iliyopanda daraja ya Njombe Mji, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sabasaba Julai 24 mwaka huu.
    Kiungo Salum Abubakar 'Sure Boy' atakwenda Mbeya na Azam FC kwa mchezo wa kirafiki na wenyeji

    Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, watamalizia mechi zake za kirafiki katika kanda hiyo kwa kukipiga na na timu nyingine iliyopanda, Lipuli ya Iringa, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Samora Julai 26 mwaka huu.
    Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amepanga kutumia mechi hizo tatu kuwatambua wachezaji wake, kwa kumpa kila mmoja nafasi ya kucheza ili kujua uwezo wao.
    Mbali na kuwajenga kimbinu, pia katika ziara hiyo ataendelea na mazoezi yake ya kuwapa kasi wachezaji pamoja na nguvu, lengo ni kutengeneza kikosi imara kitakachoweza kutikisa hapa nchini na kimataifa katika siku za usoni.
    Azam FC itaendelea kuwakosa wachezaji wake waliokuwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayojiandaa na mchezo wa marudiano kufuzu CHAN dhidi ya Rwanda ‘Amavubi’ Jumamosi hii, viungo Himid Mao ‘Ninja’ na Salmin Hoza, winga Joseph Mahundi.
    Mbali na hao, itashindwa kupata huduma ya washambuliaji wake, Mbaraka Yusuph, Shaaban Idd kwa wiki tatu zijazo, ambao bado ni majeruhi, ambao wataanza rasmi mazoezi muda wowote mwezi ujao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAENDA MBEYA KESHO KUIVAA MBEYA CITY JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top