• HABARI MPYA

  Sunday, July 16, 2017

  KILA SIKU TUNAFELI KWA SABABU YA WATU WALE WALE

  TANZANIA jana imetoa sare ya pili mfululizo nyumbani katika mechi za kuwania tiketi za Fainali za michuano muhimu Afrika. 
  Taifa Stars jana imeanza vibaya kampeni za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya mtoano.
  Matokeo hayo yanakuja kiasi cha mwezi mmoja na ushei, baada ya Taifa Stars kutoa sare ya 1-1 tena na Lesotho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 Cameroon.
  Kabla ya kuanza kwa mechi za kufuzu AFCON ya Cameroon 2019, ilionekana kama tumepangwa kundi mchekea, L pamoja na hao Lesotho na wapinzani wengine, ambao ni Cape Verde na Uganda.
  Lakini baada ya kuanza kwa sare ya nyumbani na timu iliyochukuliwa kama ndiyo dhaifu zaidi kundini, watu wameanza kukata tamaa mapema.
  Nahodha Mkuu wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji alizungumza baada ya mechi na akasema udogo wa eneo la kuchezea katika Uwanja wa Azam Complex, ulisababisha washindwe kushinda.
  Alisema wamezoea kucheza kwenye Uwanja mkubwa wa Taifa, ambao wakati wa mchezo huo ulikuwa umefungwa kwa ukarabati kuelekea mchezo wa kirafiki kati ya Everton na Gor Mahia ya Kenya uliochezwa Alhamisi.
  Na baada ya sare jana pia Kirumba, Nahodha wa kikosi cha CHAN, Himid Mao hakusita kusema ‘ubovu’ wa eneo la kuchezea Uwanja wa CCM Kirumba ulikuwa kikwazo kwao.
  Hata kama iwe anatoa kisingizio, lakini ukweli ni kwamba alichokisema Himid Mao ndicho tulichokiona wengi, hata wapinzani Rwanda walikilalamikia mapema tu.
  Na suala la ubovu wa Uwanja wa Kirumba, lilionekana mapema tu Machi mwaka huu wakati ule klabu ya Yanga inataka kuutumia kwa mechi za michuano ya klabu Afrika, wakaguzi wa CAF (Shirikisho la Soka Afrika) waliagiza marekebisho yafanyike kwanza.
  Ajabu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi alikuwa pamoja na wakaguzi hao Mwanza na akaliona hilo – lakini ameruhusu mechi ya Stars ichezwe hapo hapo.
  Mkurugenzi huyo huyo wa Ufundi ndiye aliyeruhusu mchezo dhidi ya Lesotho uchezwe Chamazi – lakini ajabu pia hata benchi la Ufundi la Taifa Stars halina sauti.
  Sasa bila shaka naye Salum Shaaban Mayanga atakuwa analalamikia Uwanja, lakini kwa nini alikubali mechi ichezwe pale?
  Timu imetoka kucheza kwenye viwanja vizuri Afrika Kusini, imecheza mpira mzuri na kupata matokeo ya kuridhisha kiasi cha kuanza kuamsha hisia za wapenda soka wa Tanzania kwa timu yao.
  Lakini baada ya kurejea nyumbani, wananchi wanaanza kukatishwa tena tamaa kutokana na uzembe wa watu wale wale kila siku, tena ambao eti wanaomba tena dhamana ya kuendelea kuongoza soka ya nchi hii.
  Ni aibu kubwa kwa Taifa. Dunia iliyoshuhudia Everton wakimenyana na Gor Mahia katika Uwanja mzuri wa Tanzania siku mbili baadaye inaona timu yetu ya taifa inacheza kwenye Uwanja wenye makorongo. Fedheha iliyoje!
  Matokeo ya jana yanamaanisha Taifa Stars italazimika kwenda kushinda ugenini mjini Kigali Julai 22 ili kusonga mbele katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani nchini Kenya, ambako itamenyana na mshindi kati ya Sudan Kusini na Uganda zilizotoa sare ya 0-0 pia juzi mjini Juba.
  Kwa hili la Uwanja pekee, sina haja hata ya kuzungumzia mambo mengine ya kiufundi, ikiwemo mfumo ‘huo huo’ wa kocha Mayanga katika kila mechi, ambavyo vinaweza kuwa sababu nyingine za kutufelisha.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA SIKU TUNAFELI KWA SABABU YA WATU WALE WALE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top