• HABARI MPYA

  Thursday, September 01, 2016

  ULIMWENGU AWAPA USHAURI MZURI YANGA SC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Emmanuel Ulimwengu amewashauri Yanga SC kujipanga kwa michuano ya Afrika mwakani ili wafike hatua ya makundi tena.
  Ulimwengu na TP Mazembe waliangukia kundi moja, B na Yanga katika Kombe la Shirikisho Afrika na timu ya Lubumbashi ikafuzu Nusu Fainali huku mabingwa wa Tanzania wakishika mkia kundini.  
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana kutoka Lubumbashi, Ulimwengu alisema kwamba Yanga walikosa uzoefu tu katika ushiriki wao wa mwaka huu, lakini anaamini mwakani wakijipanga watafanya vizuri.  
  Thomas Ulimwengu amewashauri Yanga SC kujipanga kwa michuano ya Afrika mwakani ili wafike hatua ya makundi tena

  “Mimi nilichokiona kwa haraka haraka, Yanga waliponzwa na ugeni tu na kukosa uzoefu wa mechi za makundi. Ila naamini wamejifunza mengi na kama mwakani watarudi, watafika mbali,”alisema.
  Ulimwengu amewashauri Yanga SC kujipanga kwa ajili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani ili wafike tena hatua ya makundi.
  “Tena ikiwezekana walenge kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, inawezekana kabisa, ni kujipanga tu, hii michuano yote inafanana tu, timu ni zile zile, suala ni kupata nafasi tu ya kucheza michuano hii au ile,”alisema. Mazembe imeongoza Kundi A kwa pointi zake 13 baada ya mechi sita, wakati Yanga ilimaliza mkiani kwa pointi zake nne.
  Mazembe imeungana na Mouloudia Olympique de Bejaia ya Algeria kwenda Nusu Fainali wakiipiku Medeama ya Ghana iliyomaliza nafasi ya tatu.
  Yanga ilianza michuano hiyo kwa kufungwa 1-0 na MO Bejaia nchini Algeria, kabla ya kufungwa 1-0 tena na Mazembe na baadaye sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana, mechi zote zikipigwa Dar es Salaam.
  Katika mzunguko wa pili, Yanga ikafungwa 3-1 na Medeama nchini Ghana, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Mo Bejaia Dar es Salaam na kupigwa 3-1 TP Mazembe mjini Lubumbashi.  
  Lakini tayari Yanga ina tiketi ya kucheza tena michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AWAPA USHAURI MZURI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top