• HABARI MPYA

    Friday, September 30, 2016

    AZAM WAANZIA TANGA KUSAKA VIPAJI VYA U-17, ZANZIBAR BAADAYE KIDOGO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, imefanya mabadiliko kidogo kuhusu mpango wake wa kitaifa wa kusaka wachezaji wenye umri wa miaka 17 (U-17) na sasa badala ya kwenda Visiwani Zanzibar Oktoba 8 mwaka huu, zoezi hilo limehamishiwa mjini Tanga tarehe hiyo.
    Taarifa ya Azam FC imesema kwamba kuahirishwa kwa zoezi hilo visiwani Zanzibar kunatokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao hasa baada ya Uwanja wa Amaan, Zanzibar waliopanga kufanyia majaribio hayo kuwa na matumizi mengine siku hiyo.
    Baada ya hatua hiyo, Azam FC imesema itataja baadaye tarehe nyingine ya majaribio kwa wakazi wa Zanzibar (Unguja na Pemba).
    "Hivyo, kama umezaliwa kuanzia mwaka 2000, 2001 na 2002 na unaishi mkoani Tanga, unaombwa kufika na kuonyesha kipaji chako kwenye majaribio ya nne ya wazi kuendeshwa na Azam FC yatakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani Jumamosi ya Oktoba 8, 2016,"imesema taarifa ya Azam na kuongeza; "Tafadhali unaombwa kufika na nakala ya cheti chako cha kuzaliwa kwa wale wote watakaokuja kwenye majaribio hayo,".
    Awali zoezi hilo lilimalizika kwa mafanikio makubwa mkoa wa Dar es Salaam katika Wilaya za Temeke, Kigamboni, Ilala, Kinondoni na kwa Azam FC kuvuna jumla ya vipaji 15 wataoingia kwenye fainali ya mwisho ya mikoa yote Novemba mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM WAANZIA TANGA KUSAKA VIPAJI VYA U-17, ZANZIBAR BAADAYE KIDOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top