• HABARI MPYA

    Thursday, September 29, 2016

    MAKOCHA SERENGETI BOYS WASEMA VIJANA WAKO TAYARI KWA MCHEZO WA MARUDIANO

    Na Mwandishi Wetu, BRAZZAVILLE
    MAKOCHA wa timu ya taifa ya Mpira wa Miguu ya vijana wa Tanzania ‘Serengeti Boys’, Bakari Nyundo Shime na Muharami Mohammed anayewanoa makipa watatu wa timu hii, wamesema kwa pamoja: “Tuko tayari kwa vita.”
    Shime maarufu kama Mchawi Mweusi, amezungumza hayo wakati anaendelea kufanya maandalizi ya mwisho ya mchezo dhidi ya Jamhuri ya Congo utakaofanyika Jumapili Oktoba 2, kwenye Uwanja wa Alphonse Massamba-Débat ulioko kwenye Makutano ya Barabara za Nkolo na Boko, hapa jijini Brazzaville.
    Katika mazungumzo yake, Shime anasema: “Timu iko vizuri. Tumejiandaa vizuri kwa yale ya msingi yote tumekamilisha. Kwa hivyo, kila kitu kiko sawa, kama tulivyokusudia. Tupo hapa Congo kwa sasa kumalizia au kukumbushia mambo mawili au matatu hivi.
    “Lakini pia tupo hapa Congo kuzoea hali ya hewa. Kwa bahati nzuri si tofuati na ya nyumbani Tanzania,” anasema Shime kwa kujiamini kabisa leo mchana Septemba 29, 2016 huku akijiandaa kwenye mazoezi.
    Shime anasema kwamba mfumo atakaoutumia ni wa 4-4-2 katika mchezo huo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana. Fainali hizo zitafanyika jijini Antananarivo, Madagascar mwezi Aprili, mwakani.
    Anasema kwamba mfumo huo ni rafiki kwa Serengeti Boys kwani katika michezo takribani 15 ya kimataifa hajapoteza hata mmoja, “Kwa hivyo siwezi kubadili mfumo huu. Ni mfumo wa kushambulia na kulinda tusifungwe. Vijana wanauelewa zaidi na ndio mfumo wetu.”
    Shime aliyekuwa mchezaji zamani kabla ya ndoto zake za kusonga mbele kufutwa kwa majeruhi, anasema kwamba benchi nzima la ufundi linafahamu kuwa mchezo wa Jumapili dhidi ya Congo ni mgumu kwa sababu ya umuhimu wake.
    Na akiwaelezea Congo - wapinzani wake, Kocha Shime anasema: “Ni timu ya kawaida kwa maana wanafungika. Kwenye mchezo huu ukiangalia kwa makini sisi ndio tunahitaji zaidi ushindi kuliko Congo. Lakini nataka uwaambie Watanzania kwamba pamoja na hayo, nawaheshimu Congo, najua wako nyumbani lakini mwisho wa siku ni wachezaji 11 kila upande ndio watakaoingia uwanjani.”
    Amesema kwamba amekiandaa kikosi chake vema kabisa katika eneo la mbinu, ufundi na saikolojia. “Akili za vijana wangu wooooote ni kuhakikisha tunafanya vema kwenye mchzo wa Jumapili.”
    Naye Kocha wa Makipa, Muharami Mohammed au Shilton, alisema: “Silaha zangu ziko tayari kwa vita, makipa wangu wangu wote akiwamo Kelvin Kayego, Ramadhani Kabwili na Brazio wote wako fiti. Ye yote kati yao anaweza kucheza.”
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAKOCHA SERENGETI BOYS WASEMA VIJANA WAKO TAYARI KWA MCHEZO WA MARUDIANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top