• HABARI MPYA

    Friday, September 23, 2016

    SAMATTA: NINAJISIKIA VIZURI KWA SASA, NAWEZA KURUDI WIKI IJAYO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba sasa anajisikia vizuri na ameanza mazoezi mepesi baada ya kupata ahueni ya maumivu ya goti.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kutoka Genk, Samatta aliyeumia katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa League dhidi ya Rapid Viena Alhamisi iliyopita Uwanja wa Allianz, Viena, Austria, KRG Genk ikifungwa 3-2 amesema anaendelea vizuri.
    "Najisikia vizuri kwa sasa, nimeanza mazoezi mepesi na Daktari, natarajia kurudi uwanjani kaunzia wiki ijayo," amesema Nahodha huyo wa Taifa Stars ambaye amekosa mechi mbili hadi sasa.
    Goti la Samatta lililoumia katika mchezo dhidi ya Rapid Viena wiki iliyopita
    Samatta amekosa mechi moja ya Ligi ya Ubelgiji wakifungwa 2-0 na Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk Jumapili na jana katika kombe la Ligi ya Ubelgiji, wakishinda 4-0 ugenini dhidi ya Eendracht Aalst Uwanja wa Het Pierre Cornelisstadion, Aalst.
    Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
    Katika mechi hizo, ni 14 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.
    Genk watashuka tena uwanjani Jumapili kumenyana na Kortrijk Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk katika Ligi ya Ubelgiji, kabla ya Alhamisi wiki ijayo kurejea kwenye Europa League watakapoikaribisha Sassuolo ya Italia katika mchezo wa pili wa Kundi F.
    Katika mchezo wa jana, mabao yote ya Genk yalifungwa na mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis dakika za 14, 22, 45 na 55.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA: NINAJISIKIA VIZURI KWA SASA, NAWEZA KURUDI WIKI IJAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top