• HABARI MPYA

    Wednesday, September 28, 2016

    SIMBA NA YANGA ISITUSAHAULISHE SERENGETI BOYS NA VITA YA KONGO

    JUMAMOSI wiki hii kutakuwa na mchezo mkali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, Simba na Yanga utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Huo ni mchezo mkubwa wa soka nchini, ambao huzikutanisha timu kongwe na zenye historia ndefu katika mpira wa miguu Tanzania na unapowadia mambo mengi husimama.
    Ndiyo maana hata katika mzunguko huo, mechi nyingine zote zimepelekwa Jumapili ambazo ni kati ya Mbeya City na Mwadui, Maji Maji na Stand United, Mtibwa Sugar na African Lyon, Kagera Sugar na Prisons, Azam na Ruvu Shooting na Mbao na JKT Ruvu Stars. 
    Inafahamika kuelekea mchezo wa Simba na Yanga, uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huelekeza nguvu zake zote kwenye maandalizi ya mchezo, kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kulingana na ukubwa wa mchezo wenyewe.
    Unazungumzia mandalizi ya mchezo kwa ujumla, hali ya usalama, usimamizi wa mapato na kadhalika – yote haya hufanya TFF ijipe likizo ya kushughulikia masuala mengine karibu yote ya soka nchini ili Simba na Yanga ipite salama na kwa faida.
    Bahati mbaya, Simba na Yanga ya kwanza ya msimu huu itafuatiwa na mchezo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya fainali za U-17 mwakani Madagascar, kati ya wenyeji Kongo – Brazaville na Tanzania.
    Mchezo huo utafanyika mjini Brazaville Jumapili na timu ya U-17 ya Tanzania ipo kambini Kigali, Rwanda tangu Alhamisi iliyopita baada ya mchezo wa kwanza walioshinda 3-2 nyumbani Dar es Salaam Jumapili wiki iliyopita.
    Serengeti Boys wanatakiwa kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba katika mchezo wa marudiano Oktoba 2 mjini Brazaville.
    Naamini wachezaji wa Serengeti Boys chini ya benchi la Ufundi linaloongozwa na Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa na Muharami Mohammed ‘Shilton’ wanaweza kwenda kuulinda ushindi wao wa nyumbani.
    Lakini pamoja na hayo, nataka kuwaambia TFF kwamba wasije wakapoteza dhamira yao ya kuhakikisha Serengeti Boys inafuzu fainali za Madagascar mwakani tu kwa sababu ya kujielekeza zaidi kwenye kusimamia Simba na Yanga wiki hii.
    Mchezo wa Jumapili wa Serengeti Boys ni muhimu, viongozi wa TFF wanapaswa kugawana majukumu kwa kuhakikisha baadhi yao wanashughulikia mchezo wa Kongo kikamilifu – na pia kwa Serikali, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo isisubiri kuja kutoa pongezi au shutuma, bali iwe sehemu ya vita hii. Kila la heri Serengeti Boys. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ISITUSAHAULISHE SERENGETI BOYS NA VITA YA KONGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top