• HABARI MPYA

    Wednesday, September 21, 2016

    NGASSA ASAINI MIAKA MIWILI FANJA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
    KIUNGO wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa leo amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na klabu ya Fanja ya Oman.
    Ngassa aliyesaini baada ya mazungumzo na Mwenyekiti wa klabu, Sheikh Saif Abdullah Al-Sumri mwishoni mwa wiki, ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo kwamba anafungua ukurasa mpya wa maisha yake.
    "Ninamshukuru Mungu kwa kusaini Fanja. Hii ni changamoto nyingine kwangu. Naamini kufika hapa ni mipango ya Mungu na sasa naelekeza nguvu zangu katika kukabiliana na changamoto hii mpya,"amesema leo Ngassa akizungumza kwa simu kutoka Oman ambako alitua Oman Alhamisi iliyopita. 
    Na mchezaji huyo wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba, Yanga SC, Azam FC na Simba za Dar es Salaam anajiunga na wawakilishi hao wa Oman kwenye Ligi ya Mabingwa ya Asia, kiasi cha wiki tatu tangu avunje mkataba na klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
    Ngassa alijiunga na Free State Stars Mei mwaka jana akisajiliwa na kocha Mmalawi, Kinnah Phiri kwa mkataba wa miaka minne.
    Hata hivyo, kocha aliyemsajili baba huyo wa Farida (9) na Faria (7) alifukuzwa baada ya miezi miwili tu na sasa tayari yuko Mbeya City ya Tanzania.
    Katika kipindi cha mwaka mmoja wa kuwa Free State, Ngassa alifanya kazi na makocha wanne akiwemo huyu wa sasa, Mfaransa Denis Lavagne aliyeanza kazi Juni mwaka huu.
    Wengine ni Mjerumani Ernst Middendorp aliyefanya kazi kati ya Septemba na Desemba 2015, Mtaliano Giovanni Solinas aliyefanya kazi kati ya Desemba na Mei 2016.
    Na Lavagne ndiye aliyechangia Ngassa kuomba kuondoka Free State baada ya kuonyesha kuidharau Tanzania haiwezi kuwa na mchezaji bora.
    Lavagne alimuanzishia benchi Ngassa katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya ABSA ya Afrika Kusini Agosti 23, kabla ya kumuingiza dakika ya 63 kwenda kuchukua nafasi ya Mbuyiselo Thethani wakati huo tayari FS imekwishapigwa 2-1, matokeo yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo.
    Na baada ya kuingia Ngassa akaenda kucheza kwa kiwango kizuri na kukaribia kufunga mara mbili hadi kocha huyo akampongeza baada ya mchezo, ingawa tayari mchezaji wa Tanzania alikwishatumbukiwa nyongo na Mfaransa huyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA ASAINI MIAKA MIWILI FANJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top