• HABARI MPYA

    Thursday, September 22, 2016

    SAMATTA AUMIA GOTI, GENK YAIBUTUA 4-0 EENDRACHT AALST

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta yuko nje kwa wiki moja sasa kutokana na maumivu ya goti.
    Samatta aliumia katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa League dhidi ya Rapid Viena Alhamisi iliyopita Uwanja wa Allianz, Viena, Austria, KRG Genk ikifungwa 3-2.
    Na Nahodha huyo wa Taifa Stars amekosa mechi mbili hadi sasa, moja ya Ligi ya Ubelgiji wakifungwa 2-0 na Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk Jumapili na jana katika kombe la Ligi ya Ubelgiji, wakishinda 4-0 ugenini dhidi ya Eendracht Aalst Uwanja wa Het Pierre Cornelisstadion, Aalst.
    Mbwana Samatta yuko nje kwa wiki moja sasa kutokana na maumivu ya goti

    Samatta anatakiwa kuwa nje kwa angalau wiki mbili, lakini taarifa nyingine zinasema maumivu yake ni ya kupumzika kwa wiki moja tu, maana yake anaweza kuanza mazoezi wakati wowote kuanzia leo.
    Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.
    Katika mechi hizo, ni 14 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.
    Nikolaos Karelis alifunga mabao yote jana KRC Genk ikishinda 4-0 

    Genk watashuka tena uwanjani Jumapili kumenyana na Kortrijk Uwanja wa Guldensporen mjini Kortrijk katika Ligi ya Ubelgiji, kabla ya Alhamisi wiki ijayo kurejea kwenye Europa League watakapoikaribisha Sassuolo ya Italia katika mchezo wa pili wa Kundi F.
    Katika mchezo wa jana, mabao yote ya Genk yalifungwa na mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis dakika za 14, 22, 45 na 55.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AUMIA GOTI, GENK YAIBUTUA 4-0 EENDRACHT AALST Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top