• HABARI MPYA

    Sunday, August 21, 2016

    YANGA WAWE MAKINI NA KESSY, RUHUSA YA TFF ‘INA MATEGE’

    KAMATI ya Sheria na Hadhi za wachezaji imepitia usajili wa wachezaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kumpitisha beki Hassan Ramadhani Kessy kuitumikia Yanga SC kuanzia msimu huu 2016/17.
    Kamati hiyo iliyokutana Alhamisi imechukua hatua hiyo baada ya kuona Kessy hana tatizo katika usajili, badala yake madai ambayo pande husika zinaweza kudaiana wakati mchezaji anaendeleza kipaji chake.
    Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa imepitia usajili wa timu zote na kujiridhisha kwamba suala la mchezaji Hassan Kessy limeegemea kwenye madai na si usajili ambako Simba ndiye mdai kwa kumtuhumu mchezaji huyo kuwa alianza kuitumikia Yanga kabla ya kumaliza mkataba wake Simba SC. Mkataba wake ulifika mwisho, Juni 15, 2016.

    Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Yanga SC wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya. 
    TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani.
    Kanuni hazimzuii mchezaji kuendelea kucheza kwa hoja ya madai badala yake suala hilo linaweza kumalizwa wakati mashindano yanaendelea. Kamati inaendelea kupitia malalamiko na pingamizi za wachezaji wengine na inatarajiwa kutoa taarifa rasmi kuhusu wachezaji wote wakati wowote kuanzia sasa.
    Hiyo ni kwa mujibu wa TFF na habari zaidi zinasema kwamba, katika Mkataba wa Smba, wote klabu na mchezaji walikubaliana atakayeuvunja atalipa dola za Kimarekani 60,000 zaidi ya Sh. Milioni 120,000 za Tanzania.
    Kessy alisajiliwa na Simba SC misimu miwili iliyopita kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa Mkataba wa miaka miwili akilipwa Sh. Milioni 20. 
    Meneja wa Kessy, Athumani Tippo alisema anashangazwa na uamuzi wa Kamati kumtaka Kessy ailipe Simba.
    Tippo alisema Mkataba wa Kessy na Simba uliisha Juni 17 na beki huyo wa kulia akasaini Yanga SC Juni 21, baada ya kuzungumzo ya awali kufanyika mwishoni mwa Mei.   
    “Kilichotokea baada ya habari za Kessy kutaka kuhamia Yanga kuvuja, Mei 25 mwaka huu alipokwenda kwenye mechi ya fainali ya Kombe la TFF dhidi ya Azam mashabiki wakamvisha jezi ya Yanga,”.
    “Hakuvishwa na klabu ya Yanga, ni mashabiki. Sasa huwezi kusema Kessy alivunja Mkataba na Yanga kinyume cha utaratibu,”alisema Tippo.
    Pamoja na hayo, Tippo alisema kwamba amepeleka malalamiko Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA) ili waweze kumsaidia mchezaji huyo katika sakata hilo.
    TFF wamemruhusu Kessy kuchezea Yanga, lakini wakati huo huo wanaangalia namna ya kuhakikisha Simba wanapata haki yao.
    Haki yenyewe ni Sh. Milioni 120 ambazo inadaiwa Simba na Kessy walikubaliana mapema ili kuhakikisha Mkataba baina yao unaheshimiwa. 
    Siku zote madai ya aina hii huzitokea puani klabu na nina wasiwasi kabisa, iwapo hukumu itabaki, hivi kwamba Kessy acheze, lakini ailipe Yanga ipo siku klabu hiyo ya Jangwani itaibua kilio.
    Kwa sababu ninachokiona hapa, TFF watakata fedha za Yanga zinazopitia kwao na kuilipa Simba. Yanga watafanyeje?
    Ndiyo maana ninaona kuna umuhimu wa Yanga kwanza kupata taarifa rasmi ya maandishi ya kikao cha Kamati kisha iipitie vyema, ikibidi kuomba ufafanuzi pia iwapo hawataelewa.
    Na ikibidi pia kupingana na uamuzi wa Kamati kama hawataridhika nao – lakini wakianza kufurahia sasa eti wameruhusiwa kumtumia Kessy, basi wajue iko siku watalipa Sh. Milioni 120 za Simba.
    Ni kweli Kessy aliondoka Simba baada ya kumaliza msimu, lakini kuhusu madai ambayo Simba wanasema wana ushahidi nayo alisajliwa Yanga akiwa hajamaliza Mkatabaa nao, hiyo ni kesi ya kutatua kwanza.
    Na ninawashauri hivyo Yanga kwa sababu hata taarifa ya TFF inayosema imemruhusu Kessy kuchezea Yanga, nayo haijatulia vile vile – eti ameruhusiwa, lakini ailipe Simba, kivipi? 
    Rudia sehemu hizi mbili za taarifa ya TFF, kisha tafakari kwa mapana marefu; “Kama ni madai Simba inaweza kuendelea kumdai Kessy au Yanga SC wakati mchezaji huyo anatumika uwanjani kwa mwajiri mpya,” ya kwanza hiyo. 
    Ya pili; “TFF inafuatilia na kuangalia haki ya Simba namna ya kupata haki yake baada ya kuwasilisha madai kuhusu kuvunja mkataba na mwajiri wake wa zamani,”.
    Yanga wanapaswa kuwa makini na ruhusa hii, haijatulia hata kidogo. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAWE MAKINI NA KESSY, RUHUSA YA TFF ‘INA MATEGE’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top