• HABARI MPYA

  Thursday, August 11, 2016

  SIMBA YA OMOG JUMAPILI NA URA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MASHABIKI wa Simba SC watapata fursa ya kukishuhudia kikosi chao kwa mara ya pili wiki hii, kitakapomenyana na URA ya Uganda katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  URA wanatarajiwa kuwasili leo na kesho watacheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Mapema Jumatatu, Simba SC iliitandika mabao 4-0 AFC Leopard ya Kenya katika mchezo wa kwanza rasmi wa kirafiki chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog.  
  Katika mchezo huo uliokwenda sambamba na sherehe za miaka 80 ya Simba, mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib Migomba aliendelea kumvutia kocha Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia. 
  Kikosi cha Simba SC kilichoifunga 4-0 AFC Leopard Jumatatu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
  Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Hajib dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita takriban 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Mussa Ndusha.
  Hajib alimalizia vizuri krosi ya Kichuya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 56, kabla ya Kichuya kufunga bao la tatu dakika ya 66, akimalizia krosi ya Mavugo.
  Mavugo aliyeingia kipindi cha pili kumpokea Muivory Coast Frederick Blagnon, aliifungia Simba SC bao la nne dakika ya 82 akiunganisha krosi nzuri ya Kichuya.
  Je, Jumapili Simba SC itaendeleza wimbi la ushindi katika mechi za kujiandaa na msimu mpya? Tusubiri tuone.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YA OMOG JUMAPILI NA URA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top