• HABARI MPYA

    Friday, August 19, 2016

    SAMATTA APIGA BAO MUHIMU UGENINI EUROPA LEAGUE, KRC GENK YATOA SARE 2-2 CROATIA

    Na Mwandishi Wetu, ZAGREB
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa Alhamisi ameiongoza KRC Genk ya Ubelgiji kupata sare 2-2 dhidi ya wenyeji Lokomotiva Zagreb Uwanja wa Maksimir mjini Zagreb.
    Katika mchezo huo wa kwanza wa hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Europa League, Samtta alifunga bao la pili la Genk dakika ya 47, baada ya Leon Bailey kutangulia kuifungia timu hiyo kwa penalti dakika ya 36.
    Mabao ya wenyeji yalifungwa na Mirko Maric kwa penalti dakika ya 52 na Ivan Fiolic dakika ya 59 na Genk sasa itahitaji sare ya bila mabao au ushindi mwembamba hata wa 1-0 katika mchezo wa marudiano Alhamisi ijayo Uwanja wa Luminus Arena, Genk ili kufuzu makundi.
    Mbwana Samatta wa pili kulia katika mchezo huo usiku wa Alhamisi
    Genk imefika hatua hii baada ya kuitoa Cork City FC ya Ireland kwa ushindi wa jumla wa 3-1, baada ya kushinda 1-0 nyumbani na 2-1 ugenini.
    Samatta ambaye Desemba 13 mwaka huu atafikisha miaka 24, alijiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, iliyomtoa Simba SC ya Tanzania mwaka 2011.
    Na baada ya mafanikio makubwa akiwa na klabu ya Lubumbashi ikiwemo kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwa mfungaji bora wa michuano hiyo sambamba na kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika, Samatta akahamia Ulaya Januari mwaka huu.
    Samatta amecheza mechi ya 26 katika mashindano yote, zikiwemo 18 za msimu uliopita na nne za msimu huu hadi sasa, kati ya hizo nne ni za Europa League msimu huu.
    Katika mechi hizo ni 11 tu ndiyo alianza, nyingine zote akitokea benchi na ameweza kufunga mabao saba, moja tu katika Europa League.
    Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Bizot, Walsh, Dewaest, Colley, Uronen, Heynen, Pozuelo, Ndidi, Bailey, Buffalo/Trossard dk42 na Samatta/Karelis dk82.
    Lokomotiva Zagreb: Zagorac, Peric, Majstorovic, Rozman, Bartolec, Sunjic, Bockaj/Cekici dk86, Coric/Ivanusec dk45, Fiolic, Grezda na Maric.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA APIGA BAO MUHIMU UGENINI EUROPA LEAGUE, KRC GENK YATOA SARE 2-2 CROATIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top