• HABARI MPYA

  Wednesday, August 17, 2016

  KESSY AANZISHWA YANGA NA AZAM MECHI LA NGAO…TAMBWE NA NGOMA WOTE WAMO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BEKI Hassan Ramadhani Kessy kwa mara ya kwanza ataichezea klabu yake mpya, Yanga SC katika mechi ya mashindano leo, baada ya kupangwa kwenye kikosi kinachoanza dhidi ya Azam FC.
  Kessy ameshindwa kuichezea Yanga tangu asajiliwe Juni kutoka Simba kwa sababu klabu yake ya zamani haikutoa barua ya kumruhusu baadaa ya kuondoka kinyume cha utaratibu.
  Yanga, mabingwa wa mataji yote msimu uliopita wanamenyana na washindi wa pili wa mataji yote msimu huo, Azam FC katika mchezo wa Ngao ya Jamii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni ya leo.
  Hassan Kessy (kulia) ameanzishwa kwenye mchezo dhidi ya Azam FC leo
   

  Na kocha Mholanzi Hans van der Pluijm amewaanzisha kipa Deogratius Munishi, mabeki Kessy kulia, Mwinyi Hajji Mngwali kushoto, Mbuyu Twite na Vincent Bossou katikati.
  Viungo ni Said Juma ‘Makapu’ chini, Haruna Niyonzima kulia, Juma Mahadhi kushoto, Thabani Kamusoko juu na washambuliaji Amissi Tambwe na Donald Ngoma.
  Wachezaji wa akiba ni Benno Kakolanya, Oscar Joshua, Deus Kaseke, Simon Msuva, Malimi Busungu, Matheo Anthony na Pato Ngonyani.
  Mechi hiyo itachezeshwa na refa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Ngole Mwangole wa Mbeya, atakayesaidiwa na Josephat Bulali na Frank Komba wa Dar es Salaam, refa wa akiba atakuwa Soud Lila wa Dar es Salaam pia, wakati Kamisaa Peter Temu wa Arusha.
  Pazia la msimu mpya linafunguliwa leo kwa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Yanga SC na Azam FC, ambao utakuwa mchezo wa nne kwa timu hizo kukutana mwaka huu pekee.
  Awali timu hizo zilikutana katika mechi tatu za mashindano matatu tofauti, Yanga ikishinda moja na kutoka sare mara mbili.
  Januari 5, timu hizo zilitoa sare ya 1-1 kwenye Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar, Machi 5, zikatoa sare ya 2-2 kabla ya Yanga SC kushinda 3-1 Mei 25, katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka laTanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Katika mchezo wa leo, Azam FC itakuja na benchi jipya la Ufundi chini ya makocha kutoka Hispania watupu chini ya Zeben Hernandez Rodriguez, wakati Yanga itaendelea kuongozwa na Mholanzi Hans van der Pluium anayesaidiwa na mzalendo, Juma Mwambusi.  
  Na kwa ujumla, kwenye Ngao ya Jamii hii itakuwa mara ya nne mfululizo Yanga na Azam kukutana tangu mwaka 2013. Na katika mechi zote za awali ni Yanga SC waliobuka kifua mbele dhidi ya Azam. Mwaka 2013 Yanga walishinda 1-0 bao pekee la Salum Telela, aliyeachwa msimu huu na kuhamia Ndanda FC ya Mtwara, 2014 walishinda 3-0 Mbrazil Genilson Santana ‘Jaja’ akifunga mabao mawili na mwaka jana walishinda kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.
  Yanga wataingia kwenye mchezo wa kesho wakitokea hoteli ya Tiffany katikati ya Jiji, walipoweka kambi yao, wakati Azam FC watatokea kwenye hosteli zao za Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KESSY AANZISHWA YANGA NA AZAM MECHI LA NGAO…TAMBWE NA NGOMA WOTE WAMO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top