• HABARI MPYA

  Sunday, August 14, 2016

  CHIRWA MBONA BONGE LA MCHEZAJI, YANGA WAMPE MUDA TU WATAFURAHI NA ROHO ZAO

  YANGA SC imepata ushindi wa kwanza jana katika Kombe la Shirikisho, lakini winga Obrey Chirwa alikosa mabao mengi ya wazi.
  Amesimangwa sana jana Chirwa kuanzia uwanjani hadi kwenye vijiwe na manyumbani – na bahati yake timu ilishinda, lakini kama ingetoa sare au kufungwa, angelaaniwa zaidi.
  Yanga jana imefufua matumaini ya kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria katika mchezo wa marudiano Kundi A Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Shukrani kwake, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Josleyn Tambwe aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza. 
  Ushindi huo wa kwanza baada ya mechi tano, unaifanya Yanga ifikishe pointi nne baada ya awali kufungwa mechi tatu na kutoa sare moja ingawa inaendelea kushika mkia katika Kundi A.
  Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano za sare tatu na ushindi mmoja. 
  Tambwe alifunga bao hilo dakika ya pili tu ya mchezo, akimalizia mpira uliookolewa kufuatia Simon Msuva kuunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul kutoka upande wa kulia.
  Yanga sasa inaomba Medeama ya Ghana ifungwe na TP Mazembe leo na baadaye ikatoe sare na MO Bejaia nchini Algeria ili kwenda Nusu Fainali.
  Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mnono jana, kama Chirwa angekuwa makini na kutumia vizuri nafasi zaidi ya nne za wazi alizotengenezewa.
  Nafasi iliyowasikitisha zaidi mashabiki wa Yanga ni ya kipindi cha pili, Chirwa aliporuka kichwa cha mkizi baada ya krosi ya Simon Msuva kutoka kushoto, lakini akapiga hewa akiwa amebaki na kipa, huku mpira ukienda nje.
  Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.
  Chirwa amesajiliwa mwezi uliopita tu Yanga kutoka FC Platinums ya Zimbabwe, timu ambayo wametoka wachezaji wengine wawili wa Yanga, Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko na Mzambia Donald Ngoma.
  Na jana ndiyo kwanza amecheza yake ya nne Yanga SC tangu asajiliwe, ingawa hajafunga bao hadi sasa.
  Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23 ya Zambia ni pendekezo la Ngoma kwa uongozi wa Yanga.
  Na Chirwa si mshambuliaji kama ilivyoelezwa wakati anasajiliwa Yanga, bali ni kiungo wa pembeni mwenye kasi, nguvu na krosi nzuri tu.
  Katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar timu hizo zikitoka sare ya 0-0, Chirwa alicheza nafasi yake ya wingi kulia na baadaye kushoto. Alicheza vizuri na akatia krosi nyingi nzuri. Ni winga mzuri sana ambaye anaweza kuwa mpishi mzuri wa mabao katika Ligi Kuu.
  Lakini mazuri yote aliyoyafanya katika mchezo na Mtibwa Sugar aliyatia doa jana kwa kukosa mabao ya wazi.
  Alicheza vizuri, alipambana dhidi ya  mabeki wenye nguvu wa MO Bejaia. Alionyesha uhai, aliisumbua ngome ya wapinzani, lakini mwisho wa siku akawa anakosa mabao ya wazi na hapo akaudhi mno mashabiki wa Yanga.
  Lakini turudi kumtazama Chirwa kama mchezaji ukiondoa mabao aliyokosa. Ni mchezaji mzuri? Ndiyo. Chirwa ni mchezaji mzuri ambaye pamoja na kukosa mabao jana, lakini anaweza kuja kuwa na msaada mkubwa kwa Yanga.
  Kukosa mabao wakati mwingine ni kwa sababu ya bahati tu na inaonekana kabisa Chirwa jana alicheza nyuma ya bahati yake.
  Nashawishika kuwashawishi wana Yanga wampe muda huyu mchezaji, naona mambo mazuri yanakuja kupitia kwake.
  Ni kijana mdogo na anaonekana kabisa ana kiu ya kufika mbali kisoka – kukosa mabao ni hali ya kawaida na ya kupita, ukweli unabaki pale pale, Chirwa ni mchezaji mzuri, anayestahili kupewa muda Yanga. Alamsiki.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA MBONA BONGE LA MCHEZAJI, YANGA WAMPE MUDA TU WATAFURAHI NA ROHO ZAO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top