• HABARI MPYA

  Wednesday, August 17, 2016

  AZAM FC WAIKALISHA YANGA NA KUBEBA NGAO TAIFA, KESSY NA NIYONZIMA WAKOSA PENALTI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imetwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya kwanza baada ya kuifunga Yanga SC kwa penalti 4-1 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya 90 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana mabao 2-2, ya Yanga yakifungwa Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma yote wakati ya Azam FC yalifungwa na beki Shomary Salum Kapombe na Nahodha John Raphael Bocco. 
  Katika mikwaju ya penalti, Aishi Salum Manula alipangua mkwaju wa beki Hassan Ramadhani Kessy wakati kiungo wa Rwanda, Haruna Fadhil Niyonzima alipaisha.
  Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alifunga penalti pekee na ya kwanza ya Yanga, wakati mikwaju ya Azam FC ilitumbukizwa nyavuni na Nahodha Bocco, Nahodha Msaidizi Himid Mao Mkami, Shomary Salum Kapombe na Kipre Michael Balou. 
  Wachezaji wa Azam FC wakishangilia na Ngao ya Jamii baada ya kuwafunga Yanga kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2
  Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akimkabidhi Ngao Nahodha wa Azam FC, John Bocco baada ya mechi

  Ngoma alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 20, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa na beki wa Azam FC, David Mwantika kwenye boksi.
  Mwantika tena akafanya makosa yaliyoizawadia Yanga bao la pili dakika ya 26.
  Alijaribu kumpiga chenga Amissi Tambwe, ikakataa na mshambuliaji huyo wa Burundi akaunasa mpira na kumpasia Ngoma aliyefunga bao la pili. 
  Almanusra Ngoma akamilishe hat trick dakika ya 37 baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya kiungo Juma Mahadhi, lakini ikaokolewa na kurudi na uwanjani. 
  Mpira ulimkuta Mahadhi akiwa kwenye nafasi nzuri ndani ya boksi, lakini akapiga juu ya lango na Yanga kupoteza nafasi nzuri ya kumaliza kipindi cha kwanza inaongoza 3-0.
  Kipindi cha pili, mambo yakabadilika na Azam FC wakachomoa mabao yote mawili kabla ya mchezo kuhamia kwenye matuta, ambako Yanga ‘ilifia’.
  Mshambuliaji wa Yanga, Donald Ngoma akishangilia baada ya kufunga bao la kwanza 
  Donald Ngoma akimtoka kiungo wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza
  Viungo Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam FC (kulia) na Haruna Niyonzima (kushoto) wakigombea mpira
  Nahodha wa Azam FC, John Bocco akiwatoka wachezaji wa Yanga, Said Juma 'Makapu' na Mwinyi Mngwali  
  Beki wa Azam FC, Ismail Adam (kushoto) akichuana na kiungo wa Yanga, Juma Mahadhi

  Shomary Kapombe alianza kuifungia Azam FC dakika ya 74 akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza.  
  Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ akaendelea kuonyesha umuhimu wake kwenye timu baada ya kufunga bao la kusawazisha kwa penalti dakika ya 90.
  Refa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, Ngole Wangole alitoa penalti ya pili kwenye mchezo huo baada ya beki Mtogo wa Yanga, Vincent Bossou mwenye asili ya Ivory Coast kuunawa mpira kwenye boksi.
  Azam FC inatwaa Ngao ya Jamii kwa mara kwanza baada ya kuwania bila mafanikio mara nne kuanzia mwaka 2012 ikifungwa na Simba SC 3-2, kabla ya kuanza kufungwa mfululizo na Yanga 1-0 mwaka 2013, mwaka 2014 mabao 3-0 na mwaka jana kwa penalti 8-7 kufuatia sare ya 0-0.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deogratius Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Hajji Mngwali, Mbuyu Twite, Vincent Bossou, Said Juma ‘Makapu’, Haruna Niyonzima, Juma Mahadhi/Malimi Busungu dk81, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe/Simon Msuva dk67 dk na Donald Ngoma.
  Azam FC; Aishi Manula, Isamil Adam, Bruce Kangwa, David Mwantika, Himid Mao, Jean Baptiste Mugiraneza, Shomary Kapombe, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Kipre Balou dk90, John Bocco, Shaaban Chilunda/Mudathir Yahya dk46 na Ramadhani Singano ‘Messi’/Francesco Zekumbariwa dk46. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WAIKALISHA YANGA NA KUBEBA NGAO TAIFA, KESSY NA NIYONZIMA WAKOSA PENALTI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top