• HABARI MPYA

    Friday, January 15, 2016

    FARID MUSSA APATIWA NAFASI CELTIC, ATHLETIC BILBAO…DILI LA SLOVENIA 100% SAFI, AZAM TU!

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Farid Malik Mussa anaweza kwenda Celtic FC ya Ligi Kuu ya Scotland au Athletic Bilbao ya Ligi Kuu ya Hispania kwa majaribio.
    Hiyo inafuatia wakala mmoja mwenye mahusiano mazuri na klabu hizo kuwasiliana na Azam FC, inayommiliki Farid akisema Celtic na Bilbao ndizo klabu ambazo zinahitaji mchezaji aina ya Farid.
    Na wakala huyo amefanikiwa kuishawishi Azam FC iachane na ofa ya wakala aliyekuwa anataka kumpeleka Farid klabu ya FC Olimpija Ljubljana ya Slovenia.
    Taarifa ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE imezipata kutoka Azam FC zinasema kwamba wakala huyo anayetaka kumpeleka Farid Celtic au Bilbao, tayari ametuma fedha nchini ili mchezaji huyo apate kozi za masomo ya lugha ya Kiingereza.
    Hata hivyo, mpango wa Slovenia ulikuwa ni wa mapema zaidi kwa Farid kwamba kama angekwenda Hispania kukutana na klabu hiyo kwa majaribio na kufuzu angesajiliwa katika diridha hili dogo la Januari.
    Farid Mussa amepatiwa nafasi ya kwenda Celtic ya Scotland au Bilbao ya Hispania

    Lakini haijulikani mpango wa Celtic au Bilbao kama unaweza kukamilika katika dirisha hili la usajili au baadaye.
    Na Mtanzania ambaye aliwaunganisha Azam FC na wakala wa timu ya Slovenia anaamini klabu hiyo inayomilikiwa na Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake imegoma kumuuza mchezaji huyo ili abaki kuwasaidia katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ingawa, ndani ya Azam FC wanasema wanachoangalia ni sehemu ambayo Farid akienda atapata mafanikio zaidi, lakini ukweli ni kwamba mchezaji huyo kwa sasa yuko njia panda.
    Baada ya kuzilinganisha ofa za mawakala wote wawili, Azam FC imevutiwa zaidi na yule ambaye anataka kumpeleka Farid Celtic au Bilbao.
    Lakini kutokana na mipango ya Celtic na Bilbao kuwa bado haijaiva, Farid anaonekana kutamani aruhusiwe aende FC Olimpija Ljubljana, ambako tayari mwaliko upo mezani Azam FC.  
    Ikumbukwe Farid alitarajiwa kuondoka wiki iliyopita kwenda Hispania kuungana na klabu hiyo bingwa ya Slovenia, FC Olimpija Ljubljana iliyoweka kambi huko ambako alipewa siku 10 za majaribio.
    Mabingwa hao wa Slovenia waliweka kambi nchini Hispania kujiandaa na Ligi ya kwao na Farid alitarajiwa kuwa nao kwa siku zote 10 akifanya nao mazoezi kabla ya kuamua kumununua. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FARID MUSSA APATIWA NAFASI CELTIC, ATHLETIC BILBAO…DILI LA SLOVENIA 100% SAFI, AZAM TU! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top