• HABARI MPYA

    Friday, February 01, 2019

    PRISONS YAIGONGA KAGERA SUGAR 2-0 KAITABA, KMC WATOKA SALAMA KAMBARAGE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Tanzania Prisons leo imepata ushindi wa ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Ushindi huo ulitokana na mabao ya Jumanne Elfadhili kwa penalti dakika ya 40 na Salum Kimenya dakika ya 90 na ushei, unaifanya Tanzania Prisons ifikishe pointi 20 baada ya kucheza mechi 23, ikijiinua kutoka mkiani kabisa mwa ligi hadi nafasi ya 18.
    Na huo ni mwendelezo mzuri wa timu hiyo chini ya kocha mpya, Mohammed Rishard ‘Adolph’ baada ya kuuanza msimu vibaya chini ya kocha Mohammed Abdallah ‘Bares’ aliyefukuzwa licha ya kushinda tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita.

    Kagera Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mecky Mexime yenyewe inabaki na pointi zake 28 katika mechi ya 22 ikishika nafasi ya 10.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Baraka Mtui dakika ya 85 limeipa ushindi wa 1-0 Ruvu Shooting dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani. 
    Ruvu Shooting inafikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 24 na kupanda kutoka nafasi ya 15 hadi ya 12, wakati Mbeya City inabaki na pointi zake 26 za mechi 22 katika nafasi ya 14.  
    JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni nje ya kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, mabao ya Ahmed Shiboli dakika ya 33, Hassan Matelema dakika ya 47 na Ally Bilaly dakika ya 90 na ushei.
    JKT inafikihsa pointi 29 baada ya kucheza mechi 24 ikipanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya saba, wakati Mwadui FC inabaki na pointi zake 24 za mechi 24 katika nafasi ya 16. 
    Nayo Stand United imelazimishwa sare ya 0-0 na timu ya Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC) Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga. 
    KMC inafikisha pointi 35 baada ya kucheza 23 ikiendelea kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 47 za mechi 20 na Yanga SC pointi 53 za mechi 20 – na mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 33 za mechi 14 katika nafasi ya nne, wakati Stand United inafikisha pointi 26 katika mechi 24, ikiwa nafasi ya 15 sasa.
    Ligi Kuu itaendelea kwa mchezo mmoja tu kesho, Alliance FC wakiwakaribisha Lipuli FC ya Iringa Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza kuanzia Saa 10:00 jioni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PRISONS YAIGONGA KAGERA SUGAR 2-0 KAITABA, KMC WATOKA SALAMA KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top