• HABARI MPYA

  Saturday, June 02, 2018

  YANGA SC WATAMBA WAKO TAYARI KUFANYA KWELI SPORTPESA SUPER CUP

  Na Mwandishi Wetu, NAKURU
  KIUNGO wa Yanga, Thaban Kamusoko amesema kwamba wapo tayari kwa michuano ya SportPesa Super Cup inayotarajiwa kuanza kesho mjini Nakuru, Kenya.
  Akizungumza baada ya mazoezi ya jana jioni viwanja vya Michezo vya Nakuru, Kamusoko alisema kwamba kikosi cha Yanga kina morali ya kutosha kuwavaa wapinzani wao, Kakamega Homeboys kwenye mechi ya ufunguzi.
  “Timu ipo vizuri na ina morali ya hali ya juu kuelekea kwenye mchezo wetu wa kwanza na hakika tumedhamiria kufanya makubwa kwenye michuano hii, kwani ukweli ni kwamba Yanga ni timu kubwa na inacheza ili kushinda mataji,"alisema Mzimbabwe huyo.
  Kamusoko ambaye ni Kaimu Nahodha wa Yanga kwenye michuano hiyo kutokana na kutokuwepo kwa beki Kelvin Yondan, aliyebaki Dar es Salaam amesema wataingia kwenye mchezo wao wa ufunguzi kwa kujiamini licha ya kutowajua wapinzani wao vyema.

  Meneja Uhusiano wa SportPesa Tanzania, Sabrina Msuya akimkabidhi jezi Nahodha wa Yanga kwenye michuano hiyo, Thabani Kamusoko 
  Sabrina Msuya akimkabidhi jezi na Nahodha wa Kakamega Homeboys pia, wapinzani wa Yanga kesho 

  “Hatuwajui sana wapinzani wetu lakini naamini wao wanatujua kwa sababu Yanga ni klabu kubwa na tunacheza mashindano ya Afrika kila mwaka, lakini sisi hatuwafahamu wao kiundani kwa sababu hatujawahi kuwasikia”, alisema.
  Kamusoko alisema mwaka huu wamedhamiria kuchukua ubingwa baada ya mwaka jana kutolewa kwenye hatua ya nusu fainali na AFC Leopards ya Kenya katika michuano iliyofanyika Dar es Salaam.
  “Mwaka jana hatukutilia maanani michuano hii, lakini tulikuja kujua umuhimu wake baada ya Gor Mahia kucheza na Everton kwa hiyo mwaka huu tumejipanga kuhakikisha haturudii makosa yaliyojitokeza”, alisisitiza Kamusoko.
  Faraja
  Naye kocha msaidizi wa kikosi hicho cha mabingwa mara 27 wa Tanzania Bara, Noel Mwandila amesema watafanya kila liwezekanalo kuhakikisha wanatwaa kombe hilo ili waweze kupata faraja baada ya kushindwa kufurukuta kwenye ligi ya ndani.
  “Tuna kila sababu ya kufanya vyema kwenye michuano hii ili tuweze kuwapa faraja mashabiki wetu ambao wamekuwa wakituunga mkono tangu mwanzo wa msimu”, alihitimisha.
  Yanga itakata utepe wa michuano ya SportPesa Super Cup siku ya Jumapili kwenye dimba la Afraha majira ya saa 7:00 mchana kwa kuwavaa Kakamega Homeboys ambao wanashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Kenya.
  Timu itakayofanikiwa kushinda kwenye mchezo huo wa ufunguzi itakutana na mshindi wa mechi kati ya Simba na Kariobangi Sharks kwenye hatua ya nusu fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC WATAMBA WAKO TAYARI KUFANYA KWELI SPORTPESA SUPER CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top