• HABARI MPYA

    Monday, June 18, 2018

    MWAMOYO HAMZA AKUMBUSHIA SABABU ZA ZAMOYONI MOGELLA KUITWA GOLDEN BOY

    Na Mahmoud Zubeiry, WASHINGTON
    MKUU wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VOA), Mwamoyo Hamza amesema kwamba alimpachika jina la utani, Golden Boy mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Zamoyoni Mogella baada ya kufunga bao zuri katika mechi dhidi ya Pan African mwanzoni mwa miaka ya 1980.
    Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online leo makao makuu ya VOA, Washington DC, Mwamoyo amesema kwamba alifanya hivyo wakati akiwa Mwandishi wa Habari za Michezo wa gazeti la Daily News miaka ya 1980.

    Zamoyoni Mogella (kulia) akiwa na gwiji mwenzake, Peter Tino ambao wote walimalizia soka yao Yanga 

    “Zamoyoni Mogella alikuwa mchezaji mzuri sana wakati mimi ninaandika habari za michezo katika gazeti la Daily News, sasa kuna wakati Fulani Simba na Pan African walikwenda kucheza mechi moja sikumbuki haswa ilikuwa ni Kombe la nini, lakini wanagombani Kombe Fulani,”.
    “Mechi yenyewe ilipigwa (Uwanja wa Sheikh) Amri Abeid, Arusha. Simba SC walishinda ile mechi kwa bao 1-0 na bao lenyewe lilifungwa na Zamoyoni Mogella, wakati huo beki mahiri kabisa wa Pan Africans alikuwa Jellah Mtagwa, kwa hiyo Mogella alifunga bao zuri sana, kama hivi unavyozungumza magoli ya akina Cristiano Ronaldo kwenye Kombe la Dunia,”
    “Lilikuwa ni goli zuri sana, mimi nilivyorudi Dar es Salaam kuripoti kuhusu ile mechi, nikaandika stori nzima kuhusu lile goli jinsi lilivyofungwa na wakati huo nikamuita Zamoyoni Mogella, Golden Boy kutokana na Golden Goal (Goli la Dhahabu) na ndio jina la Golden Boy lilipoanza,”amesema. 
    Mwamoyo amesema mpira wa miguu na michezo kwa ujumla nchini Tanzania ilikuwa juu miaka ya 1970 hadi 1990 mwanzoni, kutokana na Michezo ya Shule za Msingi (UMISHUMTA) na Sekondari (UMISETA) kuzalisha vipaji vingi.
    Amesema kwa sasa michezo nchini Tanzania imeshuka kutokana na zuio la michezo ya UMISHUMTA na UMISETA, jambo ambalo limesababisha kukosekana kwa vijana wenye vipaji kama ilivyokuwa enzi za akina Mogella na kabla yao.
    Mogella aliwika klabu ya Simba SC na timu ya taifa ya Tanzania miaka 1980 kabla ya kwenda kumalizia soka yake kwa mahasimu, Yanga SC mwaka 1993 na enzi zake alikuwa mshambuliaji hodari wa kufunga mabao nchini. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMOYO HAMZA AKUMBUSHIA SABABU ZA ZAMOYONI MOGELLA KUITWA GOLDEN BOY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top