• HABARI MPYA

    Sunday, June 24, 2018

    LIGI YA VIJANA ILIYOMALIZIKA ALHAMISI DODOMA IMETUONYESHA AMBAVYO SOKA YETU INAELEKEA KUZIMU

    ALHAMISI wiki hii, timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Ligi Kuu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, maarufu kama Kombe la Uhai inayoshirikisha vikosi vya pili vya klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
    Hiyo ni baada ya timu hiyo kutoka Manungu, Turiani mkoani Morogoro kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Stand United ya Shinyanga viwanja vya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) siku hiyo.
    Ni ushindi uliotokana na bao pekee la Richard William dakika ya 86 na sasa timu hiyo ya Manungu mkoani Morogoro inarithi taji lililoachwa wazi na waliokuwa mabingwa, Simba SC ya Dar es Salaam walioifunga Azam FC katika fainali mwaka jana. 

    Ikumbukwe ni Mtibwa Sugar hao hao waliowavua ubingwa Simba SC katika mchezo wa Nusu Fainali baada ya kuwachapa 1-0 pia, bao pekee la Abuu Yohana dakika ya 117, wakati Stand wao waliingia fainali baada ya kuwafunga washindi wa pili wa mwaka jana, Azam FC 1-0, bao pekee la Maurice Mahela dakika ya 32.
    Mapema katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Alhamisi, Simba SC walishinda kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 1-1 na Azam FC. Simba SC walitangulia kwa bao la Yahya Mbegu dakika ya saba, kabla ya Paul Peter kuisawazishia Azam FC dakika ya 33, hivyo kuiachia mikwaju ya penalti ichague mshindi wa Medali za Shaba Kombe la Uhai 2018.  
    Timu 16 zilishiriki Ligi hiyo iliyoanzia katika makundi manne, nyingine zikiwa ni Njombe Mji FC, Mbao FC, Kagera Sugar, Maji Maji, Yanga SC, Ndanda FC, Lipuli FC, Mbeya City, Tanzania Prisons, Mwadui FC, Ruvu Shooting na Singida United.
    Michuano hiyo imedumu kwa wiki mbili tu kuanzia Juni 9 na ilifanyika baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo Simba SC ilimaliza nafasi ya kwanza mbele ya Azam FC na Yanag SC, zote za Dar es Salaam.
    Ikumbukwe moja ya kanuni za Ligi Kuu ni klabu kuwa na kikosi cha timu ya vijana, na imeelezwa wazi kwa klabu ambayo inakosa timu ya pili inapoteza sifa za kushiriki ligi hiyo.
    Jambo zuri klabu zote zilizoshiriki Ligi Kuu nchini zimeweza kutimiza sharti hilo kwa muda wote wa uwepo wa kanuni hiyo takriban miaka 10 sasa, ingawa inasikitisha hatujaweza kuwa na michuano madhubuti ya vijana kwa kipindi chote hicho.
    Na kwa miaka kadhaa mashindano ya vijana ya wiki mbili kila baada ya msimu wa Ligi Kuu yalisimama kabla ya kurejea mwaka jana na kukawa na ahadi kwamba mwaka huu yangefanyika katika mtindo kamili wa Ligi sambamba na Ligi Kuu ya wakubwa.
    Ilielezwa timu za vijana zingesafiri sambamba na vikosi vya wakubwa zao, kwenda kucheza mechi za Ligi Kuu mikoa tofauti, lakini kwa mara nyingine imeshindikana kuwa na Ligi ya vijana na tumeshuhidia tena mashindano ya wiki mbili katika viwanja vya vumbi pale Dodoma.
    Mashindano yale yalikuja siku chache baada ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes kutupwa nje ya mbio za kuwania tiketi za Fainali za U20 Afrika baada ya kuchapwa mabao 4-1 na wenyeji, Mali Uwanja wa Omnisports Modibo Keita mjini Bamako Mei 20, mwaka huu.
    Kwa matokeo hayo, Tanzania ilitolewa katika kinyang’aniyiro cha tiketi ya Niger mwakani kwa jumla ya mabao 6-2, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Mei 13 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam ikiiacha Mali ikienda kukutana na Cameroon iliyoitoa Uganda.
    Soka ya vijana ndiyo msingi wa kuwa na wachezaji wazuri wa baadaye na kwa nchi yenye kuota mafanikio katika mchezo huo inahitaji kuwa na programu nzuri, timamu, madhubuti na endelevu za soka ya vijana kuanzia ngazi ya chini kabisa angalau chini ya umri wa miaka 13.
    Kwetu Tanzania tulichofanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kuwa na mashindano mengi kama ya kuibua vijana hivi, lakini namna ya kuwaendeleza imekuwa tatizo kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo hiyo ya kuwa na Ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 kwa wiki mbili tu.
    Baada ya mechi tatu tu za Kundi wachezaji wanakuwa wamemaliza msimu wa Ligi kama timu zao zinatolewa hatua hiyo – na kwa aliyecheza mechi nyingi ni sita pamoja na tatu nyingine za Robo Fainali, Nusu Fainali na Fainali.
    Hii inatosha kujiainisha namna ambavyo sisi ni wababaishaji tunaotaka kufanya ili tuonekane tumefanya na si kufanya ili kufanikisha azma ya kuzalisha wachezaji bora.
    Namna hii huwezi kustaajabu nchi inamtolea macho kijana Yussuf Poulsen wa Denmark anayezaliwa na baba Mtanzania, ambaye baada ya kukuzwa vizuri katika mfumo wa soka ya vijana sasa amekuwa mchezaji mzuri kiasi cha Mkurugenzi wa Michezo, Dk. Yusuphu Singo kuwashitua viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamulike vipaji vya vijana wenye asili ya Tanzania wanaocheza nje. 
    Wapo akina Yussuf Poulsen wengi sana Tanzania kama nchi itakuwa na mfumo mzuri wa soka ya vijana kuanzia kwenye kuibua vipaji, kuviendeleza na kuvitunza badala ya desturi ya sasa kutaka kujionyesha tu tunafanya na si kufanya kwa dhati.
    Lazima ifike wakati Tanzania tukome kuwa watu wa kutamani tamani, na badala yake kujiwekea utaratibu wa kutengeneza vitu vyetu wenyewe kwa matarajio ya kuvigeuza bidhaa zenye thamani siku moja.
    Huwezi kuwa na Ligi ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya wiki mbili, halafu ukaota kuwa na Ligi Kuu nzuri – ni uongo kwa sababu huo ndiyo umri ambao wachezaji wanaanza kucheza ligi kubwa duniani na hadi kufika umri wa miaka 23 wanaitwa wazoefu kabla ya kuanza kuitwa wakongwe na wazee kati ya miaka 25 na 30.
    Huwezi kustaajabu klabu za Tanzania sasa zote zinataka wachezaji kutoka nje ya nchi, hata Biashara United ya Mara na KMC zilizopanda msimu huu – kwa sababu haziridhishwi na wachezaji wa nyumbani kwa kuwa tumeshindwa kupika vipaji na sasa tunatolea macho vya wenzetu.
    Kama Simba, Yanga na Azam FC zimekuwa zikitawala soka ya Tanzania kwa sababu ya wachezaji wa kigeni, tunawezaje kuwa na Taifa Stars bora? Na sasa ndiyo imefikia hata timu zilizokuwa zinategemewa kuzitengenezea wachezaji hizo timu kubwa, nazo zinanunua wageni.
    Tutarajie nini? Msimu huu Simba imemnunua Asante Kwasi kutoka Lipuli, ambao nao walimnunua kutoka Mbao FC – ongezeko la wachezaji wa kigeni huku kukiwa hakuna mpango thabiti wa kutengeneza vipaji vya wachezaji wazawa. 
    Ndiyo maana ninasema Ligi ya vijana iliyomaliza Dodoma Alhamisi ndiyo kilelezo halisi cha soka ya Tanzania kuelekea kuzimu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI YA VIJANA ILIYOMALIZIKA ALHAMISI DODOMA IMETUONYESHA AMBAVYO SOKA YETU INAELEKEA KUZIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top