• HABARI MPYA

    Thursday, June 28, 2018

    ROONEY AJA WASHINGTON KUSAINI MKATABA NA DC UNITED

    Na Mahmoud Zubeiry, WASHINGTON
    MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester United, Wayne Rooney anatarajiwa kuwasili mjini Washington leo kusaini mkataba wa kujiunga na D.C. United mwishoni mwa wiki.
    Rooney ameposti picha akiwa kwenye ndege sambamba na maelezo; “Nakwenda Marekani” na tayari kuna taarifa kwamba anaondoka klabu yake ya Ligi Kuu ya England, Everton kuja kujiunga na timu ya Ligi Kuu ya Marekani dirisha la usajili litakapofunguliwa Julai 10.
    Gazeti la Washington Post limesema kwamba Rooney mwenye umri wa miaka 32 atakuwa mchezaji ghali zaidi atakaposaini mkataba wa miaka miwili na nusu ambao atalipwa dola za Kimarekani Milioni 13.
    Rooney anaweza kuanza mazoezi na timu yake mpya mwishoni mwa wiki hii, kwa mujibu wa gazeti la Post, ambalo limeripoti pia kwamba tayari amepatiwa kibali cha kuishi na kufanya kazi Marekani na anatarajiwa kucheza mechi ya kwanza Uwanja mpya wa Audi Field Julai 14 dhidi ya Vancouver Whitecaps.

    Wayne Rooney akiwa kwenye ndege kwa safar ya Washington kuja kujiunga na D.C. United  

    D.C. United inahitaji msaada, kwani kwa sasa inashika mkia kwenye Ligi ya MLS Kanda ya Mashariki ikiwa imekusanya pointi 10 tu katika mechi 12 na kocha Ben Olsen amesema Rooney anaweza kuwasaidia kupanda.
    Msimu uliopita Rooney alichezea klabu yake iliyomuibua utotoni, Everton akitokea Man United alikoondoka katikati ya mwaka 2017 na kuifungia Toffees mabao 11 katika mechi 40 za mashindano ikimaliza nafasi ya nane Ligi Kuu.
    Rooney amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake Everton, lakini klabu hiyo imeshindwa kupambana na msimamo wa mfungaji huyo wa kihistoria wa mabao wa timu ya taifa ya England kuhamia Marekani.
    Rooney alisaini Man United mwaka 2004, akitokea Everton kijana mdogo wa umri wa miaka 18 kwa dau la Pauni Milioni 25.6 na kwenda kuifungia klabu hiyo jumla ya mabao 253 katika mechi 559 Uwanja wa Old Trafford, akishinda mataji matano ya Ligi Kuu ya England.
    Rooney, anayeshika nafasi ya tano katika orodha ya wachezaji waliocheza mechi nyingi Man United kihistoria, pia ameshinda mataji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League, Kombe la FA na Kombe la Ligi mara tatu katika miaka yake 13 ya kuwatumikia Mashetani hao Wekunfu.
    Rooney amestaafu timu ya taifa ya England, ijulikanayo kama ‘Simba Watatu’ akiwa ameichezea mechi 119 na kuifungia 53.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ROONEY AJA WASHINGTON KUSAINI MKATABA NA DC UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top