• HABARI MPYA

    Sunday, June 03, 2018

    VIONGOZI TFF WASIPOHESHIMU MAAGIZO YA MHESHIMIWA RAIS DK MAGUFULI…


    WIKI ya mechi za kirafiki za kimataifa inahitimishwa leo kwa michezo kadhaa duniani, timu mbalimbali za taifa zikijitupa uwanjani kucheza michezo ya kuviweka sawa vikosi vyake.
    Tumeshuhudia jana England ikipata ushindi mwembamba wa 2-1 dhidi ya Nigeria, mabao yake yakifungwa na Gary Cahill dakika ya saba na Harry Kane dakika ya 39 wakati la Super Eagles lilifungwa na Alex Iwobi dakika ya 47.
    Lakini kwa Tanzania hakuna hata dalili za kuwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa katika wiki hii maalum iliyotengwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuzikutanisha timu uwanjani.
    Inafahamika kocha Salum Mayanga amemaliza mkataba wake Machi na ilitarajiwa ama mzalendo huyo kuongezwa kandarasi, au kuajiriwa kocha mwingine kuendelea kuijenga Taifa Stars kwa mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

    Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Taifa Stars itasafiri kuwafuata Uganda Septemba 7, mwaka huu kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza.
    Unaweza kuona umuhimu wa kuijenga Taifa Stars madhubuti kabla ya mechi hizo, lakini katika mastaajabu ya hali ya juu, TFF chini ya Rais wake, Wallace Karia imekaa kimya juu ya suala la kocha na sasa mipango ya Taifa Stars inaelekea kusimama.  
    Hakukuwa na ubaya kwa Mayanga kupewa mkataba mpya kama shirikisho bado halijawa na uwezo wa kuajiri kocha wa kigeni, kwa sababu rekodi yake si mbaya na pia kuendana na msemo wa Waingereza ‘Something is better than nothing’, bora kuwa nacho, kuliko kutokuwa nacho kabisa.
    Katika mchezo wake wa mwisho akiwa kocha wa timu ya taifa, Mayanga aliiongoza Taifa Stars kuifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) 2-0 Machi 27 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani.
    Huo ulikuwa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
    Na wafungaji hao wote walisetiana siku hiyo, akianza Kichuya, mchezaji aliyeibuliwa Mtibwa Sugar ya Morogoro katika timu ya vijana, kabla ya kuivutia Simba SC mwaka juzi akiwa timu ya wakubwa na kusajiliwa kwa mamilioni na baadaye Samatta akajibu.
    Tanzania iliingia kwenye mchezo huo ikitoka kufungwa 4-1 na Algeria mjini Algiers Machi 22 katika mchezo mwingine wa kirafiki na kwa ujumla huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa Taifa Stars ndani ya mechi 10, ikifungwa nne na sare tano.   
    Taifa Stars ilitoa sare mbili mfululizo na Rwanda kufuzu Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), 1-1 Julai 15 mjini Mwanza na 0-0 Julai 22 mjini Kigali, kabla ya kutoa sare nyingine za 1-1 mfululizo na Malawi mjini Dar es salaam Oktoba 7 na Benin Novemba 12.
    Ikatoa sare ya 0-0 na Libya Desemba 3, ikafungwa 2-1 mara mbili, kwanza na Zanzibar Desemba 7, baadaye na Rwanda Desemba 9 na 1-0 na Kenya Desemba 11 kwenye michuano ya Challenge mjini Nairobi.
    Matokeo haya yanamaanisha Stars inahitaji kuendelea kujengwa kwa michezo zaidi ya kirafiki kabla ya kurudi kwenye mechi za kufuzu AFCON, lakini ajabu hilo wakubwa hawajaliona na wii ya FIFA inakatika TFF wakiitazama kama haiwahusu.
    Bahati mbaya zaidi haya yanakuja wiki mbili tu tangu timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes kutupwa pembeni ya mbio za kuwania tiketi za Fainali za U20 Afrika kwa jumla ya mabao 6-2 baada ya kuchapwa 4-1 na wenyeji, Mali Uwanja wa Omnisports Modibo Keita mjini Bamako katika mchezo wa marudiano Mei 20, ikitoka kufungwa 2-1 kwenye mchezo wa kwanza Mei 13 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kabla ya kipigo hicho, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli alisema kwamba Tanzania imefungwa vya kutosha kwenye mashindano ya kimataifa ya soka na umefika wakati ianze kushinda. 
    Rais Magufuli aliyasema hayo Mei 19 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Simba SC wakifungwa 1-0 na Kagera Sugar. 
    Rais Magufuli alisema tangu taifa limepata uhuru mwaka 1961, timu za Tanzania zimekuwa hazifiki mbali kwenye mashindano ya kimataifa na akaagiza ufike wakati timu zetu ziweze kushiriki Kombe la Afrika na kombe la Dunia. 
    Alisema; “Sijawahi kuingia kwenye mpira wowote kwa sababu ya frustration ya timu zetu kushindwa. Ifike mahali tuanze kushinda, tumeshindwa vya kutosha. Ifike mahali sasa tushinde. Viongozi wa TFF, BMT na klabu tuweke mikakati ya ushindi. Ni aibu kubwa, tumesindwa vya kutosha,”.
    Katika hotuba yake siku hiyo, Rais Magufuli alionyesha ana imani kubwa na uongozi uliopo madarakani wa TFF – na hata alipowaambia kama inatoshwa kufungwa maana yake anafuatilia matokeo. Maana yake anajua kama Ngorongoro imetolewa.
    Aliposema anajua kuhusu Barcelona, tujue anafahamu kuhusu soka kwa ujumla na anajua kwamba kwa sasa kuna mechi za kirafiki za kimataifa, lakini hasikii chochote kuhusu Taifa Stars au Tanzania yake.
    TFF wanapaswa kukumbuka Mheshimiwa Rais amekuwa hajitokezi kwenye viwanja vya mpira kwa sababu ya frustration ya timu za Tanzania kushindwa – na tayari amewaagiza iwe inatosha kufungwa, hivyo wanapaswa kutengeneza mazingira ya timu kushinda.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIONGOZI TFF WASIPOHESHIMU MAAGIZO YA MHESHIMIWA RAIS DK MAGUFULI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top