• HABARI MPYA

    Saturday, June 02, 2018

    NI MTIBWA SUGAR BINGWA KOMBE LA TFF 2018, YAIPIGA SINGIDA UNITED 3-2 ARUSHA

    Na Mahmoud Zubeiry, ARUSHA
    TIMU ya Mtibwa Sugar imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Komba la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Singida United jioni ya leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Shujaa wa Mtibwa Sugar leo alikuwa ni kiungo Ismail Mhesa aliyefunga bao la tatu na la ushindi dakika ya 88 na kuamsha shangwe za mashabiki wa timu hiyo kutoka Manungu mkoani Morogoro.
    Na hiyo ilikuwa ni baada ya Singida United kutoka nyuma kwa 2-0 na kusawazisha mabao yote na kuwa 2-2 kiasi cha kupata nguvu zaidi na kuanza kutawala mchezo.
    Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (kulia) akimkabidhi Kombe la TFF, Nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi
    Ismail Mhesa akikimbia baada ya kufunga bao la ubingwa kwa Mtibwa Sugar 
    Mpira wa kona uliopigwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya' ukiwapita wachezaji wote na kudondokea nyavuni
    Salim Kihimbwa alikuwa tayari kuusindikiza nyavuni kama usingeingia wenyewe
    Wachezaji wa Mtibwa Sugar wakifurahia na Kombe lao baada ya mechi

    Na Mhesa aliifungia Mtibwa Sugar bao la ushindi dakika 10 tu tangu waanze kucheza pungufu, kufuatia beki wao wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutolewa kwa kadi nyekundu ya utata na refa Emmanuel Mwandemwa wa hapa, aliyekuwa anasaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga Ferdinand Chacha wa Mwanza.
    Mtibwa Sugar ya kocha Zuberi Katwila iliuanza vizuri mchezo huo na kufanikiwa kuongoza kwa 2-0 kwa mabao ya Salum Kihimbwa dakika ya 22 na Baba Ubaya dakika ya 37 kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 78.
    Dakika mbili kabla ya mapumziko, Singida United walizinduka na kupata bao la kwanza lililofungwa na Salum Chuku na timu hizo zikaenda kupumzika matokeo yakiwa 2-1.
    Kipindi cha pili Singida United waliokuwa wanacheza kwa mara ya mwisho chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye anahamia Azam FC waliingia kwa kasi na kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Mtibwa Sugar.
    Na haikuwa ajabu Singida United walipofanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 69 kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu – kabla ya Mhesa kupeleka Kombe la TFF Manungu.
    Mhesa akatajwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi na kukabidhiwa tuzo yake maalum na Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kabla ya Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo kuwakabidhi Kombe mabingwa.
    Mkurugenzi wa Idara ya Michezo wa Azam TV, Patrick Kahemele akamkabidhi kiungo wa Mtibwa Sugar, Hassan Dilunga tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano, wakati Meneja Masoko wa benki ya KCB, Kcb david kigwile meneja masoko alimkabidhi Habib Kiyombo wa Mbao FC tuzo ya Mfungaji wa mashindano kwa mabao yake saba.
    Kwa ushindi huo, pamoja na Kombe walilokabidhiwa na kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, Mtibwa Sugar wamepata pia donge nono la Sh. Milioni 50, kutoka kwa wadhamini Azam TV huku Singida United wakipata Sh. Milioni 40, wakati wote Dilunga na Kiyombo kila mmoja atapatiwa Sh. Milioni 1 na Mhesa Sh. 700,000. 
    Kikosi cha Mtibwa; Benedict Tinoco, Kassian Ponera, Hassan Isihaka, Dickson Daud, Shaaban Nditi, Ismail Mheja, Henry Joseph, Kelvin Kongwa, Hassan Dilunga na Salum Kihimbwa/Hassan Maganga dk89.
    Kikosi cha Singida United; Ally Mustapha, Michael Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Maliki Antiri, Kennedy Juma, Mudathir Yahya/ Danny Ussengimana dk79, Deus Kaseke, Kenny Ally, Lubinda Mundia, Tafadzwa Kutinyu na Salum Chuku
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MTIBWA SUGAR BINGWA KOMBE LA TFF 2018, YAIPIGA SINGIDA UNITED 3-2 ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top