• HABARI MPYA

  Sunday, June 03, 2018

  KUTINYU ASAINI MWAKA MMOJA AZAM FC, NGOMA AENDA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU LEO

  Na Saada Salmin, DAR ES SALAAM
  WAKATI Azam FC leo imemtambulisha rasmi mchezaji wake mpya, kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Singida United, Mzimbabwe mwenzake, Donald Ngoma aliyesajiliwa pia timu hiyo Chamazi, Dar es Salaam kutoka Yanga anaondoka leo kwenda Afrika Kusini kwa vipimo.
  Ngoma ataondoka Saa 3:45 usiku wa leo akiongozana na Daktari Mkuu wa klabu, Mwanandi Mwankemwa kwenda Capetown ambako atafanyiwa vipimo vya maumivu yaliyomuweka nje kwa msimu mzima akiwa Yanga kama amepona.
  Kwa mujibu wa makubaliano ya mchezaji huyo wa zamani wa FC Platunums ya Zimbabwe na klabu hiyo ya Aljah Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake – majibu ya vipimo hivyo ndiyo yataamua mustakabali wake Azam FC.

  Meneja wa Azam FC, Philipo Alando (kulia) akiwa na Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu baada ya mchezaji huyo kusiani hivi karibuni

  Wakati inamchukua kutoka Yanga mwezi uliopita, Azam ilisema kwamba Ngoma atasaini mkataba rasmi baada ya vipimo vya Afrika Kusini kama vitaonyesha amepona.
  Wakati huo huo, Mzimbabwe mwenzake, Kutinyu amesaini mkataba wa mwaka mmoja Azam FC wenye kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja kama atafanya vizuri katika mwaka wake wa kwanza.  
  Kutinyu mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na Singida United msimu huu akitokea Chicken Inn ya kwao, Zimbababwe.
  Tayari Azam FC imekwishamtangaza Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyekuwa akifanya kazi na Kutinyu Singida United na Ngoma Yanga SC kuwa kocha wake mpya, akichukua nafasi ya Mromania, Aristica Cioaba aliyeondolewa baada ya matokeo mabaya msimu huu. 
  Pluijm aliiongoza Singida United kwa mara ya mwisho jana ikifungwa 3-2 na Mtibwa Sugar katika fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
  Pluijm alikuja Tanzania mwaka 2014 na kujiunga na Yanga SC alikofanya kazi kwa msimu mmoja kabla ya kwenda Al Shoalah FC ya Saudi Arabia na kurejea Jangwani mwaka 2015 akafanya kazi Novemba 2016 alipohamia Singida United.
  Cioaba alijiunga na Azam FC Januari mwaka jana akichukua nafasi ya makocha Waspaniola, chini ya Zeben Hernandez Rodriguez na ameshinda taji moja moja tu, Kombe la Mapinduzi Januari mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KUTINYU ASAINI MWAKA MMOJA AZAM FC, NGOMA AENDA AFRIKA KUSINI KWA MATIBABU LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top