• HABARI MPYA

    Friday, June 01, 2018

    HIMID MAO ASAINI MIAKA MITATU PETROJET YA LIGI KUU MISRI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Azam FC, Himid Mao Mkami amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Petrojet ya Ligi Kuu ya Misri.
    Himid aliyeibukia timu ya vijana ya Azam FC mwaka 2011, yupo mjini Suez nchini Misri tangu juzi na jana amesaini mkataba kuanza kazi chini ya kocha Hassan Shehata.
    Himid amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa kumaliza msimu salama na Azam FC na sasa yuko tayari kwa changamoto mpya Misri.
    "Nawashukuru Makocha, viongozi na wafanyakazi wote wa Azam FC kwa kufanya kazi pamoja kila siku kwa ushirikiano katika kupanda na kushuka, huzuni na furaha na bado walikua bega kwa bega na mimi miaka yote,"
    "Ni huzuni kusema kwaheri, lakini haikuwa na jinsi nilikwishafanya maamuzi na kushirikiana na uongozi wa Azam FC ukaniruhusu nilipoomba ruhusa ya kutafuta changamoto mpya,".
    "Nimeishi kama mwana familia kwa miaka yote, nilikuja nikiwa kijana mdogo kabisa wa kidato cha kwanza, ninaondoka nikiwa nimepevuka kimwili na kiakili, mimi ni binadamu kama kuna sehemu niliwakosea naombeni mnisamehe na mimi nimesamehe kama mlinikosea,"alisema Himid katika waraka wake wa kuaga.
    Kwa upande wake, Msemaji wa klabu, Jaffar Iddi alisema kwamba Himid ameondoka kwa baraka za uongozi; “Uongozi sisi hatuna kipingamizi, Himid ni mchezaji wetu wa muda mrefu tokea akiwa mdogo kabisa ameshiriki mafanikio mengi ya timu, mara baada ya kuleta maombi hayo sisi tulimkubalia na tunamtakia kila la kheri huko aendako katika maisha yake mapya,” alisema.
    Himid Mao Mkami amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Petrojet ya Ligi Kuu ya Misri

    Mao ni miongoni mwa wachezaji aliyecheza kwa muda mrefu Azam FC, wengine wakiwa ni John Bocco ‘Adebayor’ aliyehamia Simba SC msimu uliopita, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Agrey Moris, Mwadini Ally.
    Safari yake ndani ya Azam FC ilianza mwaka 2008 akianzia kwenye kituo cha kukuza vipaji cha Azam FC ‘Azam FC Academy’ wakati huo akiwa mwanafunzi wa sekondari, alikuwa akicheza soka huku akiendelea na shule.
    Kiungo huyo kiraka anayesifika kucheza kindava na kuharibu mbinu za wapinzani, amepitia historia ndefu ndani ya timu hiyo tokea akiwa ngazi ya chini ya Azam Academy, akiwa kama nahodha aliiongoza kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana ‘Uhai Cup’ mara mbili mfululizo.
    Katika historia yake ya maisha ya soka, Himid ameweza kuwa kiongozi uwanjani kama nahodha wa vikosi vyote vya timu za Taifa za Vijana (U-17 hadi U-23) hadi za wakubwa na vilevile kuanzia msimu hadi anaamua kuondoka amekuwa nahodha wa Azam FC.
    Kiungo huyo hadi anaondoka Azam FC, amefanikiwa kucheza jumla ya mechi rasmi 246 za mashindano mbalimbali, za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzani Bara (VPL) zikiwa 179, CECAFA Kagame Cup (8), Mapinduzi Cup (29), Kombe la ASFC (10), Ngao ya Jamii (5).
    Mbali na mechi hizo, akiwa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee wa Azam FC aliyecheza mechi zote za mashindano ya Afrika (CAF Club Competition), akiwa amecheza jumla ya michezo 15, mechi mbili zikiwa za Ligi ya Mabingwa Afrika na 13 za Kombe la Shirikisho Afrika.
    Himid ambaye ni mtoto wa nyota wa zamani wa Taifa Stars na Pamba ya Mwanza, Mao Mkami ‘Ball Dancer’, ametwaa jumla ya mataji saba rasmi akiwa na Azam FC, taji moja ya Ligi Kuu msimu 2013/2014, timu hiyo ikilitwaa kwa rekodi ya kutofungwa mchezo wowote.
    Mataji mengine aliyobeba ni Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) mwaka 2015, ikilibeba kwa rekodi ya aina yake ya kutopoteza wala kuruhusu nyavu zake kutikiswa hadi sasa ikiwa ndio bingwa mtetezi wa taji hilo, pia ametwaa Kombe la Mapinduzi mara nne na Ngao ya Jamii mara moja.
    Msimu uliopita alitwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Azam FC (NMB Player Of The Month) mwezi October-Novemba.
    Wakati huo huo: Azam FC imesema kwamba kocha mpya, Mholanzi Hans van der Pluijm atajiunga na klabu baada ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Azam Sports Federation (ASFC) akiiongoza kwa mara ya mwisho klabu yake ya sasam Singida United.
    Pluijm ambaye timu yake, Singida United kesho itamenyana na Mtibwa Sugar katika fainali ya ASFC, anakuja Azam FC kuchukua mikoba ya Mromania Aristica Cioaba, aliyekuwa na kikosi hicho msimu uliopita.
    “Kwa sasa tumeamua kumtangaza baada ya kukubaliana naye kila kitu, mambo mengine tutayaweka wazi Jumatatu ijayo, na kingine kuanzia msimu ujao Azam FC itakuwa kampuni ikijulikana Azam FC Company Limited,” alisema.
    Azam FC inaamini ya kuwa Pluijm ana uzoefu wa kutosha wa soka la Kimataifa na Tanzania utakaoisaidia timu hiyo, akizifundisha kwa mafanikio Singida United na Yanga aliyeipa mataji ya ligi, FA Cup na kuifikisha hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Kabla ya kutua Yanga, Pluijm aliwahi kuzifunza Ashanti Gold, Medeama na Berekum Chelsea zote za Ghana.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIMID MAO ASAINI MIAKA MITATU PETROJET YA LIGI KUU MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top