• HABARI MPYA

    Sunday, August 13, 2017

    MUASISI WA LIGI KUU BARA AFARIKI DUNIA, NI MZEE CHABANGA DYAMWALE

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MUASISI wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Mzee Chabanga Hassan Dyamwale amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu. 
    Dyamwale, kiongozi wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amefariki dunia akiwa ana umri wa miaka 76 baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda.
    Mtoto wa marehemu, Ngade Dyamwale na kiungo wa zamani wa Yanga SC, ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba msiba upo nyumbani kwa marehemu, Kinondoni B.
    Ngade aliyechezea pia Prisons ya Mbeya, amesema kwamba siku za mwisho za uhai wake, marehemu aliacha wosia akifariki akazikwe Handeni, ambako pia alizikwa mama yake mzazi.
    Chabanga Hassan Dyamwale amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu

    Na Ngade amesema kwamba mazishi yanaweza kuchelewa hadi mtoto mwingine wa marehemu, Mamdoe anayeishi Marekani awasili Jumanne. “Kuna uwezekano mkubwa marehemu akasafirishwa Jumatano mapema kwa mazishi yatakayofanyika Handeni,”amesema.   
    Ngade amesema baba yao ameacha wake wawili, Asha na Mboni na watoto tisa, ambao pamoja na yeye mwenyewe na Mamdoe, wengine ni Ibrahim, Mwanahija, Yahya, Mkufu, Makileo, Mkebene na Juma. 
    Umaarufu wa marehemu ulianzia kwenye mchezo wa Riadha na aliwahi kuiwakilisha Tanzania kwenye Michezo ya Olimpiki mwaka 1964 nchini Japan wakati huo akiwa na umri wa miaka 23 akiwa na akina Psacal Mfyomi, Daniel Thomas na Omar Abdallah.
    Ndiye aliyefanikisha mfumo wa ufutaji madeni ya FAT aliouita OFUMA na akaanzisha Ligi ya timu sita zikiwemo Yanga, Simba, Coastal Union, African Sports, Pamba zilizocheza ligi hiyo Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) na kufanikiwa kulipa madeni. 
    Awali kabla ya kuanzisha ligi hiyo, aliulizwa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (sasa marehemu) ataondoaje madeni ya FAT akamweleza mipangilio yake na kupewa Kombe la ushindani na Mwalimu Nyerere ambalo lilibebwa na Coastal Union, kipindi hicho Waziri wa Michezo alikuwa Jenerali Mirisho Sarakikya.
    Ni Sarakikya aliyempeleka Dyamwale kuwa Katibu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), chini ya Mwenyekiti Alhaj Said El Maamry kuanzia miaka ya 1970. Aliondoka FAT mwaka 1978 na akaenda kuwa Mkurugenzi wa Michezo nchini mwanzoni mwa miaka ya 1980.
    Mzee Dyamwale ambaye aliwahi pia kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa mpenzi na mwanachama wa klabu ya Yanga. Mungu ampumzishe kwa amani marehemu Hassan Chabanga Dyamwale. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUASISI WA LIGI KUU BARA AFARIKI DUNIA, NI MZEE CHABANGA DYAMWALE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top