• HABARI MPYA

    Monday, August 28, 2017

    MSUVA APIGA BAO KOMBE LA MOROCCO, JADIDA YASHINDA 3-1

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva, jana ameisaidia timu yake, Difaa Hassan El-Jadida kufuzu kwenye Raundi ya Pili ya michuano ya Kombe la Ligi Morocco, maarufu kama Throne Cup baada ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya CR Khemis Zemamra Uwanja wa Grand Prix mjini Marrakech.
    Msuva aliyejiunga na Difaa Hassan El-Jadida mwezi uliopita kutoka kwa mabingwa wa Tanzania, Yanga SC jana alifunga bao la tatu dakika ya 62 katika mechi yake ya kwanza rasmi ya mashindano.
    Simon Msuva wakati anaingia uwanjani kwa ajili ya mchezo wa jana
    Simon Msuva akiwa mstarini Uwanja wa Marakech jana
    Kikosi cha Difaa Hassan El Jadida kilichoanza jana

    Hiyo ni baada ya beki Marwan Aghudy kufunga bao la kwanza dakika ya 28 na mshambuliaji Bilal Almkra kufunga la pili dakika ya 34.
    Kwa ujumla, Msuva alicheza vizuri jana kushangiliwa na mashabiki wa timu hiyo ambao tayari wameanza kuimba jina lake jukwaani.
    Huu ni mwendelezo mzuri wa Msuva kufunga mabao tangu amejiunga na timu hiyo akifunga mabao sita kwenye mechi za kirafiki, zikiwemo za ziara ya Hispania.  
    Msuva alisaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na DHJ Julai 28, mwaka huu baada ya kucheza  Yanga ya nyumbani, Tanzania tangu mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro.
    Awali ya hapo, Msuva alipitia akademi ya Azam akitokea kituo cha kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi, Wakati Ujao baada ya kuibuliwa na iliyokuwa taasisi ya Pangollin ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye sasa ni Katibu wa Yanga, klabu aliyoichezea na kuifundisha awali.. 
    Na baada ya kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mfungaji bora mara mbili – Msuva amehamia Morocco kusaka changamoto mpya na mafanikio zaidi kisoka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA APIGA BAO KOMBE LA MOROCCO, JADIDA YASHINDA 3-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top